Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Felician Mtahangerwa amesisitiza umuhimu wa wana Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendelea kuwa wamoja na kutunza utamaduni wa Afrika Mashariki ili kuchochea na kukuza maendeleo ya kikanda.
Mhe. Mtahengerwa ametoa kauli hiyo leo Jumatano Agosti 14, 2024 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda, wakati alipowapokea vijana kutoka nchi saba za Afrika Mashariki, wanaozunguka nchi za Afrika Mashariki kwa kutumia Baiskeli katika kueneza ujumbe wa kusisitiza kuhusu amani na mashirikiano ya jumuiya ya EAC.
"Nimetaarifiwa kuwa mtakimbia zaidi ya Kilomita 6000, mtatumia siku 56 na kwasasa mshakimbia Kilomita 1390, hongereni sana.Jambo hili mnalolifanya ni jambo la kizalendo sana, kwanza tumeambiwa mnatumia gharama zenu na meseji mnayoipeleka ni kubwa sana kwa wana Afrika Mashariki" amesema.
Kwa upande wao Vijana hao waliotokea nchini Burundi na kisha Mkoani Manyara, wakielekea Nchini Kenya, wameshukuru kwa mapokezi mazuri waliyoyapata Mkoani Arusha, wakiahidi kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa amani na mshikamano wa EAC.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa