Wanawake mkoani Arusha wameendelea kuonyesha mshikamano na ushiriki mkubwa katika michezo na shughuli mbalimbali zinazoelekea kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, inayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka.
Katika maandalizi hayo, michezo kama rede, kuruka kamba, na mbio za kuvaa mfuko imekuwa kivutio kikubwa, huku wanawake wa rika zote wakijitokeza kwa wingi kushiriki. Mkuu wa Mkoa wa Arusha amepongeza juhudi hizo na kumuahidi Bibi Arafa Matoke ambae ni mshindi kwa upande wa mchezo wa kukimbia na gunia bajaji pamoja na runinga.
Mbali na michezo, wanawake wa Jeshi la Polisi nao wameungana na jamii kutoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia, wakihimiza jamii kushirikiana katika kupinga vitendo vyote vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto.
Wananchi walioshiriki wamesifu maandalizi ya mwaka huu, wakisema kuwa yamekuwa na msisimko wa kipekee, huku shughuli mbalimbali zikiandaliwa kwa ajili ya kuhamasisha usawa wa kijinsia na haki za wanawake. Wamesema kuwa sherehe za mwaka huu zimeleta mshikamano mkubwa na kuonyesha umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika nyanja zote za jamii.
Siku ya Wanawake Duniani ni fursa kwa wanawake kote duniani kusherehekea mafanikio yao, kujadili changamoto wanazokabiliana nazo, na kuweka mikakati ya kuimarisha nafasi yao katika jamii. Mkoa wa Arusha umeendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa namna unavyosherehekea siku hii kwa matukio yenye tija kwa jamii.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.