Zaidi ya mabehewa 800 ya mizigo kununuliwa yakiwemo yenye majokofu ili kurahisisha usafirishaji wa maua na mbogamboga ndani na nje ya nchi.
Ahadi hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akizundua rasmi usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam hadi Arusha kupitia Tanga na Kilimanjaro, katika stesheni za Reli Jijini Arusha.
Amesema wakulima wakubwa wa maua na mbogamboga wapo katika Mkoa wa Arusha hivyo atawarahisishia wafanyabiashara hao katika kupata soko la ndani na nje kupitia reli hiyo.
Amesisitiza zaidi katika maboresho ya huduma za reli nchini, serikali yake itanunua vyichwa vya treni vipatavyo 36 na mabehewa 37 ya abiria.
Amewataka watanzania kujiamini kuwa wanaweza kufanya mambo makubwa ya maendeleo katika nchi yao,hivyo wailinde na kuitunza reli hiyo ili iweze kuwanufaisha vizazi hadi vizazi.
Rais Magufuli amesema treni hiyo inamanufaa makubwa katika kukuza uchumi wa nchi,kupunguza bei za usafarishaji wa abiria na mizigo na kuokoa muda wa usafirishaji.
Akisoma taarifa ya mradi wa ufufuaji wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Arusha Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Reli Tanzania bwana Masanja Kadogosa, amesema treni hiyo ilisimamisha huduma zake tokea mwaka 1986 na sasa serikali ya awamu ya tano imetumia bilioni 14 kurudisha huduma hiyo katika mikoa hiyo ya Kaskazini.
Kadogosa amesema, tokea huduma hiyo kurejeshwa takribani tani 2600 za mizigo zimeshasafirishwa ndani ya mwezi mmoja na abaria wapatao elfu 55 wameshatumia usafiri huo kutoka Dar es Salaam hadi Arusha.
Aidha, amesema usafiri huo wa treni umelenga kutoa huduma kwa wananchi wote hususani wananchi wa kawaida na wafanyabiashara wadogo, ndio maana na hata bei zake zinakidhi hali ya mtanzania.
Nae Theresia Mollel Mkazi wa Jiji la Arusha, amesema kurejeshwa kwa huduma hizo za treni kwa Mkoa wa Arusha kutawasaidia wao kama wakazi kupunguza gharama za usafiri kutoa Dar es Salaam hadi Arusha na pia itawasaidia kuokoa muda wa kusafiri barabarani.
Theresia ameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kurejesha huduma hiyo ya treni na maendeleo mengine yote yaliyofanywa na awamu hiyo.
Uzinduzi wa treni ya abiria na mizigo Kanda ya Kaskazini umefanywa rasmi baada ya huduma hiyo kuadimika zaidi ya miaka 30 na uzinduzi huo umeshihudiwa na viongozi mbalimbali wa serikali na dini.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa