Na Elinipa Lupemne
Waziri Mkuu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) amezindua mashine ya kuchanganya virutubisho kwenye vyakula wakati akitembelea mabanda ya maonesho muda mchache kabla ya kufunga Mkutano Mkuu wa Tisa wa Wadau wa Lishe nchini uliofanyika katika Hoteli ya Mount Meru mkoani Arusha.
Akizungumza wakati wa akizindua mashine hiyo, Mhe. Majaliwa amesema kuwa serikali inaunga mkono juhudi zilizofanya na shirika hilo na kutumia fusra hiyo kuwaomba wadau wa maendeleo kuunga mkono juhudi hizo ili mashine hizo ziweze kuuzalishwa kwa wingi na kutumika nchi nzima.
Mashine iliyozinduliwa inatumika kuongeza virutubisho muhimu katika vyakula hususan unga wa mahindi, virutubisho hivyo ni pamoja na vitamin B na folic acid vinasaidia kwenye ukuaji wa watoto na kuzuia kuzaliwa na changamoto za ulemavu ikiwemo mgongo wazi na vichwa vikubwa.
“Ninawapongeza wadau walishiriki kufanikisha teknolojia hii muhimu kwa afya za watanzania, ninatambua mchango wa Shirika la GAIN, SIDO na DIT kwa kuwezesha kazi hii kukamilika, niwaombe tuendelee kusimamia vipaji vya watanzania ili kuwa na mashine zinazotengenezwa ndani ya nchi.” Amesema
Aidha Mhe. Majaliwa amewasisitiza watanzania kutumia virutubisho vinavyozalishwa nchini, sambamaba na kuwahimiza wadau kuendelea kuzalisha kwa wingi malighafi za virutubisho hivyo ili kuondokana na utegemezi wa kuviagiza kutoka nje ya nchi na kuwahakikishia wadau kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuunga mkono juhudi hizo na kuzisimamia ili kuhakikisha zinakuwa endelevu.
Awali Waziri Mkuu amesisitza Ofisi ya Rais - TAMISEMI kuhakikisha kuwa mikataba ya lishe, inatekelezwa kikamilifu na kuwa na tija kwa kufuatilia kwa karibu na kutoa taarifa za utekelezaji mara kwa mara kwa kila ngazi kama mkataba unavyoainisha ili kufikia malengo ya serikali ya kuondokana na utapiamlo na udumavu unaotokana na lishe duni.
#ArushaFursaLukuki
#kaziinaendelea
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa