Elinipa Lupembe, Arusha
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, anatarajiwa kufungua Mkutano Mkuu wa 14 wa Taasisi ya Maboresho ya Serikali za Mitaaa Tanzania (TOA), unaotarajia kufanyika mkoani Arusha kuanzia tarehe 12 - 14 Juni, 2024.
Taarifa hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa TOA Taifa na Katibu Tawala Mkoa wa Katavi, Albert Msovella, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo Juni 10, 2024 na kuweka wazi kuwa, Mkutano huo utafanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), ukibeba dhima ya uboreshaji na utendaji kazi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Amesema kuwa, mkutano huo utahusisha Makatibu Tawala wa mikoa yote 26, Wakurugenzi watendaji wa majiji, miji na halmashauri zote 184, huku wakiwalikwa na Maofisa Utumishi wa Sekritarieti za mikoa na halmashauri zote nchini pamoja na wakurugenzi wa Manispaa zote na wasimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa upande wa Zanzibar, lengo likiwa ni kuwa na uelewa wa pamoja na kubadilishana uzoefu katika utoaji huduma kwa wananchi kupitia Maamlaka hizo.
"Mkutano huu una lengo la maboresho ya Serikali za mitaa katika masuala ya ugatuaji wa madaraka kwenda kwa wananchi, ukiwemo ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo maji, kilimo, afya, miundombinu, usimamizi wa rasilimali watu, fedha na utawala bora". Amesema Msovela
Aidha, Msovella amebainisha kuwa, umoja huo ulianza mwaka 2002 kwa kushirikiana na Serikali ya Japani, kupitia Shirika la Maendeleo la kimataifa la Japani (JICA) ambapo watumishi zaidi ya 6,000 wamenufaika kwa kupata mafunzo kupitia TOA.
Awali Mkutano huo, wenye kauli mbiu ya Boresha Msingi wa Utoaji Huduma za Serikali za Mitaa, utabeba mada mbalimbali zinazotarajiwa kuwasilishwa na Maofisa wabobezi wastaafu na waliopo Serikalini.
Ofisi ya Rais - Tamisemi Ikulu Mawasiliano Samia Suluhu Kwanza Ofisi ya Waziri Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa