Waziri wa afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amesema Serikali ya Zanzibar imejipanga kuweka mfumo sawa katika sekta ya Afya ili kudumisha zaidi Muungano.
Ameyasema hayo alipofanya ziara ya kikazi katika Hospitali ya Wilaya ya Arumeru na Jiji la Arusha.
"Tushirikiane katika kubadilishana mafunzo na uzoefu baina ya Serikali hizi mbili ili kudumisha undugu zaidi".
Amesema bado kuna kazi kubwa katika sekta ya Afya hasa katika kudhibiti vifo vya mama na mtoto ifikapo 2030, hivyo ushirikiano ni muhimu.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amesema katika sekta ya Afya Serikali ilitoa kiasi cha bilioni 3.5 fedha za tozo za miamala zakujenga miundombinu mbalimbali ya Afya kama vile Hospitali za Wilaya,majengo ya wagonjwa wa nje na vifaa.
Mhe.Mongella amesema ushirikiano uliopo wa Serikali hizi mbili ni kwasababu agenda ni moja ya kuleta maendeleo kwa nchi zetu.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango amesema, Serikali ya awamu ya sita imeleta fedha za maendeleo ikiwa ni pamoja na fedha za tozo ambapo kwa Halmashauri hiyo Serikali katika sekta ya afya ilitoa Milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la kitengo cha dharura EMD , Shilingi Milioni 500 kwaajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mareu , Shilingi Milioni 90 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya watumishi Zahanati ya Maji ya chai.
Mhe.Mazrui amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Arusha kwa lengo la kuona namna mfumo unavyofanya kazi katika sekta ya Afya.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa