Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda amewataka wananchi kuyaenzi na kuyaendeleza mambo yote mazuri yaliyofanywa na hayati Edward Lowassa katika kipindi chote cha utumishi na maisha yake ya kawaida.
Hayo ameyasema leo Februari 16,2024 Monduli mkoani Arusha wakati akiongoza wananchi wa Arusha viongozi wa kiserikali na viongozi wa kimila kutoa heshima zao za mwisho kwa Hayati Edward Lowassa ambaye anatarajiwa hapo kesho Februari 17.
Amesema katika kipindi chote cha uhai wake alikua akipenda kufanyakazi kwa bidii na kuhakikisha inatimia kwa wakati hivyo ni vyema kuendelea kumkumbuka kwa kuyaenzi hayo aliyoyaweka.
“Mimi niliwahi kufanya kazi chini yake akiwa Waziri mkuu na mara zote alikuwa kiongozi ambae akisimamia jambo ni lazima litimie tutaendelea kumkumbuka kwa mengi na kuyaiga yale mazuri aliyokuwa akifanya”Amesema Pinda.
Kwa upande wake waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera,uratibu na Bunge Jenista Mhagama amesema hayati Lowassa kuna mambo mengi ameyaacha kama alama hivyo ni jukumu la serikali kuhakikisha linayaendeleza.
Naye, aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Arusha ambae ni mmoja wa marafiki wa familia ya Lowasa Paraseko Kome amesema wataendelea kumkumbuka kwa upendo,ubunifu,uchapakazi na uzalendo kwa taifa hivyo nchi imempoteza mtu muhimu.
Mwili wa hayati Edward Ngoyai Lowassa unatarajiwa kuzikwa kiserikali Februari 17 kijijini kwake Ngarash wilayani Monduli mkoa wa Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa