_Aagiza Wananchi kupewa elimu ya utunzaji wa vyanzo vya Maji_
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla ameiagiza Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Wilaya ya Karatu kuongeza kasi katika mchakato wa kumpata Mkandarasi wa kupeleka Maji kwenye Matenki pamoja na usambazaji wa maji kwa wananchi wa Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha kutoka kwenye chanzo cha Maji cha Bwawani.
CPA Makalla ametoa maelekezo hayo leo Jumatatu Septemba 22, 2025 Mjini Karatu kwenye ziara yake ya kukagua utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo, akitembelea na kukagua chanzo cha Maji cha Bwawani, Karatu Mjini, Chanzo ambacho kiliharibiwa na Mafuriko ya Mvua na kuathiri upatikanaji wa maji Karatu na hivyo kulazimu serikali kutenga fedha ili kunusuru chanzo hicho cha Maji ambacho kimekuwa tegemeo la uzalishaji maji kwa Mji wa Karatu pamoja na maeneo ya jirani.
Mhe. Makalla pia ameipongeza Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Karatu kwa usimamizi mzuri wa utoaji wa huduma za Maji kwenye Wilaya hiyo ambao umefikia asilimia 71 kwasasa, akihimiza Jamii pia kushirikishwa na kupewa elimu katika utunzaji wa vyanzo vya maji vilivyopo kwenye maeneo yao.
"Niwasihi tushirikiane pia na wananchi wa maeneo haya kuona kwamba tunatunza vyanzo vya maji lakini pia na sisi wenyewe kama Mamlaka ya Maji kuendelea kutoa elimu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na kutokuchafua vyanzo vya maji." Amesisitiza CPA Makalla.
Awali katika taarifa yake, Meneja wa Mamlaka ya Maji Karatu Injinia Steven Siayi, amemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa serikali imeshatoa zaidi ya Milioni 145 kwaajili ya kufikisha maji kutoka kwenye chanzo hicho kwenda kwenye tenki la ujazo wa maji Lita 225, 000 na baadae kusambaza Maji kwa wananchi, akisema kisima hicho kilichonusuriwa kina uwezo wa kuzalisha Maji Lita 28, 000 kwa saa.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa