_* Awahakikishia wananchi Amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi Uchaguzi*
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla @amosmakalla leo Jumatano Septemba 24, 2025 amewahakikishia amani, usalama na utulivu wanafunzi, Walezi na wananchi wa Mkoa wa Arusha katika kipindi chote cha Kampeni, siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi Mkuu wa Jumatano Oktoba 29, 2025.
CPA Makalla ameyasema hayo kwenye Viunga vya Ofisi yake Jijini Arusha wakati alipopokea maandamano ya wanafunzi wa shule ya Msingi Green Valley ya Mkoani Arusha ambao wapo kwenye shamrashamra za kuelekea kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya shule hiyo, Ujumbe wa Maadhimisho hayo ukiwa ni kusisitiza kuhusu amani kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
"Nataka niwahakikishie kuwa mtasoma kwa amani, mtaishi kwa amani na uchaguzi utafanyika kwa amani. Tunawahakikishia kwamba kuanzia sasa, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi nchi yetu itaendelea kuwa na amani na niwapongeze kwa kuadhimisha miaka 25 kwa kuhamasisha amani. Mkasome kwa amani na nchi yetu itaendelea kuwa na amani." Amesisitiza Mhe. Makalla.
Awali katika maelezo yao wanafunzi hao wameeleza kuwa wameamua kufanya matembezi hayo ya amani wakitambua kuwa amani ndio msingi wa elimu, maendeleo na ustawi wa jamii, wakisema bila amani elimu hukwama na mustakabali wao watoto hushindwa kufahamika, wakisema ni muhimu kila mmoja kufahamu kuwa kudumisha amani ni jukumu la kila mwananchi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa