_Amshukuru Mhe.Rais Dkt.Samia kwa kutoa Milioni 900 kuboresha miundombinu Hospitali ya Wilaya ya Meru_
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla @amosmakalla amemshukuru Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mapinduzi makubwa kwenye sekta ya afya Mkoani Arusha, huku Hospitali ya Wilaya ya Meru Wilayani Arumeru ikipokea shilingi Milioni 900 zilizotolewa kuboresha miundombinu ya huduma za afya hospitalini hapo.
CPA. Makalla ameyaeleza hayo leo Jumanne Septemba 09, 2025 alipotembelea na kukagua hali ya utoaji na uoatikanaji wa huduma kwenye majengo mapya manne ya Hospitali hiyo ikiwemo Jengo la wagonjwa wa nje, Jengo la Maabara, Jengo la Bohari ya dawa pamoja na jengo la kuchomea taka pamoja na jengo la wagonjwa wa dharura, majengo ambayo tayari yameanza kutoa huduma kwa wagonjwa, yakitajwa kupunguza muda wa utoaji wa huduma kwa mgonjwa kutoa saa nane hadi saa mbili.
"Faida za uwekezaji huu mkubwa ni pamoja na kupunguza masaa ya kuwahudumia wagonjwa kutoka saa nane mpaka saa mbili, uwepo wa vipimo 38 ambavyo vimepunguza rufaa za wagonjwa kwenda kwenye hospitali za rufaa kama vile KCMC na Mount Meru, haya ni mafanikio makubwa kwa serikali yetu, niwaombe watoa huduma wote kupitia uwekezaji na maboresho haya, vitafsiriwe kwa ninyi kutoa huduma bora kwa wagonjwa, kuanzia mapokezi, lugha nzuri mpaka kwenye huduma za matibabu." Amesema CPA. Makalla.
Aidha, CPA Makalla, amesisitiza kuwa, mapinduzi hayo makubwa kwenye sekta ya afya yameambatana na ongezeko kubwa la bajeti kwaajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba katika hospitali hiyo pamoja na ukarabati wa jengo la watoto njiti na watoto wachanga wenye kuhitaji uangalizi maalumu.
Awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Elisante Fabian licha ya kumuahidi Mkuu wa Mkoa kutoa huduma bora kwa wagonjwa, ameeleza faida za maboresho hayo ni pamoja na kuongeza wigo wa utoaji wa huduma, ongezeko la idadi ya wagonjwa na mapato ya Hospitali, upatikanaji wa vipimo vyote 38 sambamba na kupunguza muda wa kuhudumia mgonjwa.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa