Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amewahimiza wakazi wote wa mkoa huo waliojiandikisha, kujitokeza kwa wingi kupiga kura hapo kesho Jumatano Novemba 27, 2024 ili kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa watakaoshirikiana na Viongozi wengine kujileta maendeleo kwenye maeneo yao.
Mhe. Makonda ametoa wito huo leo Novemba 26, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Jiji la Arusha kwenye Soko la Kilombero wakati wa ufanyaji wa usafi kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni siku moja kabla ya siku ya upigaji wa kura ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amekwisha tangaza kuwa siku hiyo itakuwa ni mapumziko ili kuwaruhusu wananchi kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huo.
Mhe. Makonda amesema Viongozi sahihi na bora watasaidia katika jitihada za kutokomeza uhalifu, migogoro ya ardhi na changamoto nyingine za kijamii, akiwataka pia kutorubuniwa kushiriki kwenye Ulinzi wa kura, kwani jukumu hilo kwa utaratibu linasimamiwa na Mawakala wa Vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi huo.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa