Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu Mkoani Arusha, wametakiwa kusimamia nidhamu na maadili kwa wanavyuo na wakufunzi katika vyuo vyao kwa kufuata utaratibu wa vyuo vyao.
Yamesemwa hayo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha mheshimiwa Idd Kimanta alipokuwa akizungumza na wakuu wa vyuo vya elimu ya juu vilivyopo katika mkoa wa Arusha.
“Nendeni mkaongeze nguvu katika kusimamia nidhamu na maadili kwa wanavyuo na wakufunzi ili kukuza kuwanga cha ufaulu katika vyuo vyenu na hii itainua kiwango cha ufaulu cha mkoa kwa ujumla”,alisema.
Katibu Tawala Mkoa wa Arusha bwana Richard Kwitega, akitoa neno la ukaribisho kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa Idd Hassan
Kimanta (Aliye kaa chini) kwa wakuu wa vyuo vya elimu ya juu (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Kimanta amesisitiza zaidi ushirikiano uendelee kati ya vyuo hivyo na serikali yao ya mkoa ili kuleta maendeleo katika sekta ya elimu na uchumi kwa ujumla, kwani vyuo hivyo ni moja ya chanzo cha mapato ya uchumi kwa kutoa ajira kwa watu na hata mzunguko wa fedha zake unainua pato la mkoa.
Aidha, amewataka wawe huru kuleta mawazo yao au changamoto katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa, na hii itasaidia kuwa na ushirikiano wa karibu na kuleta maendeleo katika sekta ya elimu.
Akisisitiza zaidi Kimanta amesema hata taka kusikia aina yoyote ya migogoro katika vyuo vyote vya mkoa wa Arusha na hasa itakayotokana na itikadi za kisiasa kwani vyuoni ni mahali pakutoa elimu tu.
Baadhi ya wakuu wa vyuo vya elimu ya juu Mkoani Arusha wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Idd Kimanta (hayupo pichani)
alipokuwa akizungumza nao katika kikao kazi, kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha.
Pia, amewataka wakuu hao wa vyuo kuendelea kutoa elimu kwa wanafunzi na wakufunzi juu ya kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Corona kama inavyoelekezwa na watalaamu wa afya.
Alimalizia kwa kusema yote hayo yatawezekana ikiwa tu kutakuwa na usimamizi mzuri wa nidhamu na maadili kwa wanafunzi na wakufunzi wao.
Nae Katibu Tawala Mkoa wa Arusha bwana Richard Kwitega amesema, serikali ya mkoa wa Arusha imekuwa na itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu zaidi katika kuvisaidia vyuo hivyo kutekeleza majukumu yao na taaluma iendelee kupanda zaidi katika ngazi ya Taifa.
Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Utawala kutoka chuo kikuu cha Tumaini Makumila Profesa Faustin Mahali,ameishukuru serikali kwa kuchukua uthubutu wa kuruhusu vyuo kufungulia baada ya kufungwa kwa muda wa miezi 3 kutokana na janga la ugonjwa wa Corona.
“Tunaishukuru sana serikali kwa kuthubutu kuchukua maamuzi ya kuruhusu vyuo kufunguliwa na sasa vyuo vyetu vinauhai tena.”
Profesa Mahali amemkaribisha mkuu wa mkoa kutembelea vyuo vyote vya mkoa wa Arusha ili aweze kujionea namna elimu inavyoendelea katika ngazi hiyo ya elimu ya juu.
Baadhi ya wakuu wa vyuo vya elimu ya juu Mkoani Arusha wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Idd Kimanta (hayupo pichani)
alipokuwa akizungumza nao katika kikao kazi, kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha.
Nae Makamu Mkuu wa chuo upande wa Utawala na Fedha kutoka chuo cha Habari Maalumu bi. Astele Ndaluka amesema, wataenda kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa ili vyuo viwe na nguvu ya kutoa wanachuo walio bora katika soko la ajira.
Mheshimiwa Kimanta amekutana na viongozi hao wa vyuo kwa lengo la kujitambulisha kwao na kuomba ushirikiano kutoka kwao katika kutekeleza majukumu yake kama kiongozi wa mkoa.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa