Mkuu wa Mkoa wa Arusha Idd Hassan Kimanta, amesema viongozi wa Mkoa wa Arusha watairinda treni kwa uhakika na kuiweka salama.
Ameyasema hayo alipokuwa akipokea treni ya abiria ya majaribio iliyotoka Dar es Salaam mpaka Arusha.
Treni hiyo ilisimamisha huduma zake takribani miaka 30 iliyopita, hivyo ni furaha sana kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha kuipokea treni hiyo kwa mara nyingine tena.
Kimanta amesisitiza,treni hiyo itakuza uchumi wa Mkoa kwa kurahisisha upatikanaji wa bidhaa na marighafi mbalimbli kwa gharama nafuu zaidi.
Pia, treni hiyo itaokoa muda wa safari hasa kwa wajasiliamali katika kusafirisha marighafi zao.
Akitoa taarifa fupi ya mradi wa kufufua treni, mkurugenzi wa shirika la reli Tanzania bwana Masanja Kadogosa, amesema treni hiyo niya majaribio kwa mujibu wa sheria ya usafirishaji.
Mradi huo wa ufufuaji wa treni umegharimu kiasi cha bilioni 14 kwa reli yenye urefu wa kilometa 644.8, ambapo reli hiyo kwa mara ya kwanza ilijengwa mnamo 1929.
Katibu itikadi na uwenezi Taifa wa chama cha mapinduzi (CCM) bwana Humphrey Polepole, amesema chama kimekuja kuhakikisha treni hiyo imefika salama katika mikono ya wananchi wa Mkoa wa Arusha.
Amesema,maendeleo hayo yameletwa na serikali ya awamu ya tano kwa kuhakikisha huduma za usafiri zinaboreshwa katika nchi na hasa Mkoa wa Arusha.
Ufufuaji wa treni hiyo ulianza 2017 kwa treni hiyo kuanza safari zake kutoka Dar es Salaam hadi Moshi na 2020 treni hiyo imefika Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa