*_Latajwa kuondoa changamoto ya Maji kwenye Mtaa wa Kimindorosi, Rc Makalla akipiga marufuku ubambikiaji wa ankara za Maji*_
Wananchi wa Mtaa wa Kimindorosi Kata ya Olasiti Mkoani Arusha wameishukuru serikali kwa hatua za haraka za ujenzi wa Tenki jipya la Maji katika Mtaa wao litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi maji Lita 50,000 na hivyo kuondoa changamoto ya maji kwenye eneo hilo iliyotokana na jiografia ya Mtaa huo kuwa mlimani na hivyo kuathirika na upatikanaji wa maji pale mahitaji yanapokuwa makubwa kwenye maeneo ya tambarare.
Leo Septemba 24, 2025, wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa Mhe. CPA Amos Makalla ya kukagua miundombinu na utoaji wa huduma ya Maji kwa wananchi wa Jiji la Arusha, Mhandisi Justine Rujomba, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA), amemueleka Mkuu wa Mkoa na wananchi hao kuwa tenki hilo jipya la Maji litaanza kujazwa maji usiku wa leo na kuanza kuhudumia wananchi wa eneo hilo na hivyo kumaliza kabisa changamoto ya Maji kwenye Mtaa huo.
Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Kimindorosi Bw. Amani Saruni amesema Mtaa wake umekuwa ukikabiliwa na changamoto ya Maji hasa msimu wa kiangazi kutokana na mahitaji makubwa ya eneo hilo na Jiografia ya Mtaa wake, akisema kujengwa kwa tenki hilo kunaenda kuondoa changamoto ya Maji kwenye Mtaa huo na kutoa hakikisho la Maji ya Uhakika na salama katika vipindi vyote
Awali wakati wa maelekezo yake Mhe. Makalla amebainisha kuwa amejiridhisha na uzalishaji wa maji kwenye Jiji la Arusha, akielekeza wananchi hao kupata maji safi na ya uhakika kama ilivyoahidiwa, akipiga marufuku pia ubambikiaji wa ankara za maji kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha.
"Natoa maelekezo tufanye kazi tuhakikishe maji yamejazwa na kesho maji kwa wananchi iwe bwerere katika eneo hili. Hili tenki hapa ni kwaajili yenu ili kuwapa uhakika wa maji naombeni muendelee kutoa ushirikiano kwa mamlaka ya Maji na kutunza miundombinu hii ya Maji." Amesema Mhe. Makalla.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa