Watendaji wa Kata na Vijiji wametakiwa kuacha kutatua matukio ya ukatili wa kijinsia kienyeji badala yake wafuate Sheria ili wahusika wachukuliwe hatua kisheria zaidi.
Yamesemwa hayo katika ufunguzi wa kikao cha wadau cha tathimini ya mpango wa Taifa wa udhibiti wa ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA) na Mchumi Mkuu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa bwana Moses Mabula kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa Dkt.Athumani Kihamia.
" Watendaji wa kata na vijiji ndio walinzi wa maeneo yao hivyo ni aibu kama watatua changamoto hizo kienyeji badala ya kufuata Sheria".
Bwana Mabula amesema kikao hicho kiwe chachu ya kupata uzoefu kutoka kwa maafisa maendeleo ya kata ambao wao ndio wanaokutana na wahanga wa matukio hayo ya ukatili wa Kijinsia kwa karibu zaidi.
Aidha, amesisitiza zaidi katika kikao hicho wajumbe hao waibue changamoto zote ili zisaidie kwa ngazi ya Mkoa kupata elimu yakuweza kuipeleka katika halmashauri zingine.
Amesema kwa Halmashauri ya Arusha jumla ya Matukio 4510 yameripitiwa katika vyombo mbalimbali, hivyo Mkoa unahitaji kujifunza zaidi kutoka kwa maafisa hao ili wigo wa utoaji elimu uweze kufika mbali zaidi.
Vilevile amezitaka kamati zote za
MTAKUWWA ngazi ya Halmashauri na kata kuhakikisha Matukio yanatolewa taarifa katika vituo husika ili kulinda haki za wanawake na watoto.
Nae, mratibu wa mpango wa MTAKUWWA ngazi ya Mkoa Bi. Erena Materu amesema lengo kubwa la kikao hicho ni kufahamu mafanikio na changamoto zilizopo katika ngazi za kata na vijiji na kutafuta mbinu za kuzitatua.
Kuna juhudi kubwa zimefanyika katika kuhakikisha elimu inawafikia walengwa, Afisa ustawi wa Jamii Mkoa bwana Daniel Kasikiwe amesema jumla ya klabu 625 katika shule ya msingi zimeanzishwa kwa lengo la kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto na klabu 212 katika shule za Sekondari.
Pia, bwana Daniel amesema asilimia 43 ya kamati zimeshapatiwa mafunzo ya namna ya kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto ambacho ni kiwango kidogo sana kwa ngazi ya Mkoa.
Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Silvia Mamkwe amesema athali ni kubwa zinazotokana na ukatili wa kijinsia ikiwemo umaskini kwani wengi wanashindwa kuzalisha na wengine wanakata tamaa ya kuanzisha familia kutokana na madhara wanayokuwa wameyapata.
Dkt.Silvia ametoa wito kwa Jamii kushiriki kupinga ukatili wa kijinsia kwani ni jukumu la Jamii nzima sio kazi ya polisi na dawati la Jinsia pekee.
Mratibu wa mradi wa familia kutoka shirika binafsi la SOS bi Erena Mwakalile amesema kupitia mradi huo wameweza kuzisaidia familia nyingi kujikwamua kiuchumi kwa kuwapa elimu na kuwawezesha katika mitaji ili kupunguza ukatili wa kijinsia kwa familia kuwa maskini.
Kikao cha tathimini cha mpango wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto kimefanyika kwa halmashauri ya Arusha chini ya shirika la SOS kwenye mradi wa familia ulioanza mwaka 2008 katika halmashauri hiyo na kushirikisha maafisa maendeleo ya Jamii ngazi ya kata na halmashauri.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.