Mkoa wa Arusha umetoa tahadhari kwa wakuu wa shule zote kutotoza michango ya ziada kwa wanafunzi kwa kisingizio cha ugonjwa wa Corona pindi shule zitakapofunguliwa.
Akitoa maelekezo hayo kaimu katibu tawala msaidizi idara ya elimu Emmanuel Maundo,amesema kumekuwa na baadhi ya shule kutangaza kuchangisha wazazi fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya kujikinga na Corona.
Amesema Mkoa unaendelea kufanya ukaguzi katika shule na vyuo ili kujiridhisha na maandalizi yanayoendelea kabla ya kupokea wanafunzi mapema mwishoni mwa mwezi huu.
Maundo amesema, mkoa unasisitiza kwa wakuu wa shule zote kufuata maelekezo waliyoyatoa katika kipindi hiki cha maandalizi, ikiwemo shule zote na vyuo kuhakikisha kuna vyanzo vya maji vya kutosha ili kuwawezesha wanafunzi kunawa kila mara.
Pia,Usafi ufanyike vizuri katika mabweni na madarasa huku wakizingatia ukaaji wa mita moja au zaidi kati ya mwanafunzi na mwanafunzi na uwekaji wa vitakasa mikono katika maeneo ya madarasa, mabwalo ya chakula, mabweni,ofisi za walimu na vyooni.
Amesisitiza pia kwa walimu kutowataka wanafunzi kuja na vitu kama malimao na Tangawizi kama kigezo cha kuwapokea wanafunzi mashuleni na vyuoni.
Mkoa unawasisitiza wazazi kuhakikisha wanafunzi wote wanawasili katika shule zao kuanzia Mei 29 hadi 30,2020 na kuanza masomo mapema Juni 1,2020 kama serikali ilivyotoa mwongozo.
Aidha, wanafunzi wote wanatakiwa kuchukua taadhiri kama maelekezo ya watalaamu kutoka wizara ya afya yanavyoelekeza katika kujikinga na ugonjwa huu wa Covid 19.
Mkoa wa Arusha mpaka sasa unajumla ya shule za sekondari za kidato cha sita 57 na vyuo vya ualimu 8 na jumla ya wanafunzi 3948 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha sita kwa mwaka 2020 na wanachuo 529 kutoka katika vyuo vya ualimu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.