Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda, ameutangazia umma kuwa uwanja wa ndege wa Arusha ambao ulikuwa unatumika kwa safari za ndani tu, sasa utatumika kwa safari za nje ya Nchi ili kurahisisha Mkoa huo kufikika kirahisi.
Mhe. Makonda ametoa kauli hiyo leo Juni 16, 2025 wakati akitembelea uwanja huo na kusema hiyo ni hatua kubwa itakayoondoa changamoto ya kupoteza muda mwingi barabarani hasa kwa wafanyabiashara pamoja na wageni wanaotoka nje ya nchi kwa shughuli za utalii.
"Nilimuomba Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuruhusu uwanja wetu huu wa Arusha tupokee wageni kutoka nje angalau hata kwa ndege ndogo na kwa mapenzi yake aliruhusu na nikawasiliana na watu wa Uhamiaji, Mamlaka ya viwanja vya ndege pamoja na TRA". Amesema.
Kwa upande wake Meneja wa uwanja wa ndege Arusha Edga Mwankuga, ameahidi kuendelea kusimamia utoaji wa huduma bora kulingana na miongozo na taratibu ili kuwaridhisha wateja wao.
Hata hivyo, baadhi ya wageni waliowasili kutoka nchi mbalimbali wamefurahia huduma hiyo, huku wakipendekeza kwa wageni wengine kutua na kuondokea katika uwanja huo kwani ni rahisi zaidi.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.