Mkoa wa Arusha kuwa mwenyeji wa mashindano ya michezo kwa shule za Msingi na Sekondari kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ali maalufu kama FEASSSA.
Akizungumza na waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha,Katibu tawala wa Mkoa wa Arusha Richard Kwitega amesema mashindano hayo yatafanyika kuanzia Agosti 15,2017 hadi Agosti 25,2019.
“Mashindano haya ni fursa kubwa sana kwa Mkoa wetu wa Arusha na nchi kwa ujumla kwani inatupa nafasi yakukuza na kudumisha ushirikiano kwa nchi za Afrika Mashariki”.
Kwitega amesema Mkoa wa Arusha unatarajia kupokea wanamichezo takribani 3500 kutoka katika nchi 6 za Afrika Mashariki na nchi ya Malawi kushiriki kama mwalikwa.
Aidha, tofauti na wachezaji hao Mkoa utapokea wageni mbalimbali wakiwemo viongozi mbalimbali, Wazazi, Walimu na Waamuzi wapatao 1500 katika mashindano hayo.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi Agosti 16,2019 katika viwanja vya Sheik Amri Abeid na yataendelea kutimua vumbi katika viwanja vingine kama vya shule ya St. Costantine, Viwanja vya International School of Moshi (ISM),viwanja vya Magereza,Tigiti na ukumbi wa michezo wa Palot.
Amesisitiza kuwa michezo itakayo shindanishwa ni mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa magongo, mpira wa mikono ,mpira wa kikapu, riadha, mpira wa wavu,mashindano ya kuogolea,mpira wa meza, mpira wa kengele utakaowahusisha watu wenye ulemavu.
Kwitega, amewahamasisha wananchi wote kutumia fursa hiyo katika kukuza uchumi kwa nyanja mbalimbali zikiwemo za Utalii,Hoteli na Usafiri kwa maendeleo ya watu na nchi kwa ujumla.
Pia, wananchi wajitokeze zaidi katika viwanja hivyo ili kuweza kuburudika na kushangilia timu za Tanzania kwani ni mara ya pili mashindano hayo yanafanyika hapa nchini tokea mwaka 2014.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.