ARUSHA NA URUSI ZAKUBALIANA KUSHIRIKIANA KWENYE KUKUZA SEKTA YA UTALII NCHINI.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amekutana na kuzungumza na Balozi wa Urusi nchini Tanzania Mhe. Andrey Avetisyan na kukubaliana kuendelea kushirikiana katika kukuza Utalii wa Arusha na kuvutia wawekezaji wengi zaidi raia wa Urusi kuja kuwekeza Mkoani Arusha.
Kwenye mazungumzo yao, Mhe. Makonda amemuambia Balozi huyo wa Urusi kuwa Mkoani Arusha zipo Fursa mbalimbali za uwekezaji kwenye Hoteli za Kitalii, Kumbi za Mikutano, kwenye sekta ya Kilimo pamoja na uwekezaji kwenye usafiri wa Anga kutokana na mahitaji makubwa ya usafiri huo mkoani Arusha unaotokana na wageni na watalii wanaofika Mkoani Arusha.
Balozi Avetisyan kando ya Ratiba zake nyingine, Leo alhamisi Oktoba 17, 2024 anakutana na wafanyabiashara na Wawekezaji wa Kirusi waliopo Mkoani Arusha kwa lengo la kuwashirikisha fursa zilizopo Mkoani Arusha ambapo Mhe. Makonda pia ameahidi kushirikiana na Wawekezaji hao katika kurahisisha mazingira ya ufanyaji biashara Mkoani hapa na kusema kuwa Ofisi yake ipo wazi muda wote katika kuhudumia wageni na wenyeji wa Mkoa huo ulio muhimu kwa Utalii, biashara na shughuli mbalimbali za kidiplomasia.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.