Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Wilaya ya Longido kuilinda miundombinu ya Maji ambayo serikali imewekeza fedha nyingi.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la stendi mpya, Longido mjini.
Kwa yeyote atakaebainika kuhujumu miundombinu hiyo basi hatua kali za kisheria atachukuliwa.
Sambamba na mkutano amezindua mradi wa Maji katika Wilaya hiyo ya Longido uliogharimu bilioni 15 fedha za Serikali.
Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha Wilaya hiyo inapata Maji maeneo yote ifikapo Januari 2022 hasa katika mji wa Namanga.
Miradi yote inayotekelezwa ni fedha za Serikali zilizotokana na kodi za wananchi hivyo itunzwe na kulindwa kwa umakini.
Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso, amesema jumla ya miradi 53 ya Maji inaletwa Mkoani Arusha itakayo gharimu bilioni 16.
Amesema miradi hiyo yote imelenga katika kuhakikisha Maji yanapatikana Mjini na Vijijini kwa urahisi zaidi na kumtua Mama ndoo kichwani.
Nae, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amemshukuru Rais Samia kwa kufanya ziara Mkoani Arusha na kukagua baadhi ya Miradi katika Jiji la Arusha, Arumeru na Wilaya ya Longido.
Aidha, Mhe.Mongella ameaidi kuendelea kuisimamia na kuilinda miradi yote ambayo serikali imetoa fedha zake takribani Bilioni 12.7 kwa Mkoa wa Arusha.
Mhe. Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku 2 Mkoani Arusha, ambapo alikagua mradi wa Maji Wilaya ya Arumeru ambao ni moja ya kisima cha mradi unaogharimu Bilioni 520, amefungua Hospitali ya Jiji la Arusha iliyogharimu Bilioni 2.5, amezindua kiwanda cha Nyama Londigo kilicho gharimu Bilioni 17 na akazindua mradi wa Maji Longido uliogharimu Bilioni 15.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.