AUWSA WAPEWA SIKU TATU, KUBORESHA BARABARA YA MSASANI KATA YA MURIET JIJI LA ARUSHA.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji jiji la Arusha (AUWSA), Mhandisi John Ndetico kurekebisha miundombinu ya barabara ya Msasani kata ya Muriet, Jiji la Arusha, iliyoharibika kufuatia mvua kubwa iliyonyesha, usiku wa kuamkia 13 Novemba 2023.
Imesemekana kuwa, kutokana na kazi ya uwekaji wa miundombinu ya maji taka inayoendelea, iliofanywa na Mamlaka ya Maji, imesababisha baadhi ya maeneo kutitia na kutengeneza mashimo makubwa na maji kuingia na kujaa kwenye makazi ya wananchi wa eneo hilo.
Kufuatia uharibufu huo, Mhe. Mongella ametoa maagizo hayo wakati akitembelea barabara hiyo na kujionea madhara yaliyotokana na mvua kubwa na kumuagiza Kaimu Mkurugenzi huyo kukamilisha kazi hiyo kwa viwango vinavyokubalika kwa muda wa siku tatu.
Amemtaka kushirikiana na Viongozi wa kata hiyo huku akitoa rai kwa wananchi wanaishi maeneo hayo kuchukua tahadhari dhidi ya mvua zinazoendelea kunyesha pamoja na kuwasimamia watoto wasipate madhara kwenye maeneo hayo yaliyoharibika.
"Wazazi na walezi kuweni makini kuangalia watoto wenu wasije kuzama maana barabara zimetitia muwe makini ili maafa mengine yasije tokea"
Naye Mhandisi Ndetico amesema mkandarasi aliyepewa mradi huo,Sinohydro Corporation Ltd alishamaliza muda wake hivyo Auwsa itafanyia kazi changamoto hiyo ili tatizo hilo lisiweze kujirudia tena.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa maeneo yaliyokumbwa na changamoto hiyo, wameiomba serikali kufuatilia kwa ukaribu na kukagua miradi wanayotekeleza na wakandarasi kabla ya kuikabidhi kwa Serikali na kugundua kasoro kama hizo kabla ya madhara kutokea.
“Hii barabara ilikuwa inatumika vizuri bila changamoto lakini baada ya AUWSA kuanza kuchimba ndipo changamoto hizi zimeanza kutokea licha ya kumlalamikia mkandarasi aliyekuwa anafanya kazi hii lakini hakutusikiliza”. Amesema Herieth Steven Marunda, Mkazi wa msasani
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Msasani, Rashid Chidi, amesema kuwa awali wakati AUWSA wanachimba mifumo wa maji taka walieleza changamoto ya barabara kuharibika na lakini haikufanyiwa kazi lakini kwakuwa mvua zimenyesha na zimeonyesha tatizo hilo sasa litafanyiwa kazi kwani barabara zimegeuka mahandaki na wakati mwingine kuhatarisha usalama wa watoto wadogo na watu wazi.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.