KAIRUKI: SIMAMIENI ZOEZI LA UCHUNGUZI WA AWALI WA WATOTO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Angellah Kairuki amewaagiza Maafisa elimu Maalum wote nchini kuhakikisha wanasimamia zoezi la uchunguzi wa awali wa watoto ili kubaini watoto wenye mahitaji maalum katika jamii.
Ameyasema hayo leo tarehe 12 Disemba, 2022 wakati akifungua mafunzo kwa maafisa elimu watu Wazima na maafisa elimu Maalum iliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha Ualimu Patandi, Mkoani Arusha.
Amewataka kuhakikisha wanatumia vituo vya uchunguzi (Education Support Resource Assessment Centre) na kuwaelekeza watoto wenye mahitaji maalum katika shule stahiki ambazo wanapaswa kupelekwa ili wapate afua stahiki
Waziri Kairuki ameelekeza shughuli za usimamizi na uendeshaji wa elimu zihusishe kikamilifu masuala ya elimu maalumu na elimu ya watu wazima kwa kuhakikisha wanashirikiana na viongozi katika jamii katika kuratibu shughuli za elimu ya watu wazima na elimu Maalum katika shule za msingi na Sekondari
Ametoa rai kwa Maafisa hao kuweka utaratibu wa kupokea wanafunzi wenye mahitaji maalum wa kidato cha kwanza, darasa la kwanza na awali kwa mwaka 2023 kwa kushirikiana na viongozi katika maeneo yao ili kuweka mazingira bora kwa wanafunzi hao
Waziri Kairuki amewataka viongozi wa elimu katika ngazi ya shule, Kata, Halmashauri na Mikoa kufuatilia ufundishaji na ujifunzaji shuleni na kushirikiana na walimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata umahiri uliokusudiwa badala ya kukaa ofisini.
Aidha,ameagiza kila mwalimu lijiwekea malengo binafsi katika masomo anayofundisha na kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeshindwa kupata umahiri uliokusudiwa katika somo lake ifikapo mwishoni mwa kila mwaka
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.