Balozi wa Singapore nchini Tanzania Douglas Foo, akiungumza kwenye kikao cha fursa za Uwekezaji kwenye Mamlaka za Hifadhi za Taifa (TANAPA) kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Ngorongoro Jijini Arusha na kuahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuwekeza kwenye sekta ya Utalii.
Katika kikao hicho Balozi Foo amepata fursa ya kusikiliza fursa zinazopatikana Tanzania zilizowasilishwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kikao chenye lengo la kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini, hususani kwenye maeneo hayo ya Hifadhi za Taifa.
Hata hivyo, Balozi huyo ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuhifadhi rasilimali za asili licha ya uharibufu mkubwa wa mazingira unaoendelea duniani na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania sanjari na kuwaeleza wananchi wa Singapore juu ya fursa zinazopatikana Tanzania kwenye Sekta ya Utalii ili waweze kuwekeza, lengo likiwa ni kuongeza pato la wananchi na serikali zote mbili.
"Arusha ni eneo zuri lenye nafasi kubwa yenye uoto wa asili inayosababisha hali ya nzuri ya hewa, Arusha kuna vivutio vingi vya Utalii vinavyohifadhiwa vizuri, ni mara yangu ya kwanza kufika Arusha lakini nimevutiwa na ukarimu wa wakazi wa Arusha na hali ya hewa nzuri, ninaifananisha Arusha na nchi yangu ya Singapore kwa utajiri wa rasilimali za asili, nimekuwa na safari nzuri kufika Arusha" Amebainisha Balozi Foo.
Kikao hicho, kimejumuisha wajumbe kutoka Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, TAWA na AICC, Sekretariet ya mkoa wa Arusha na Jijini Arusha, ambapo wamewasilisha vivutio mbalimbali vya uwekezaji kwa Balozi huyo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.