Mwenyekiti wa chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha Mhe.Zelothe Steven amewaagiza Wakala wa Barabara Wilaya ya Ngorongoro (TANROAD), wathaminishaji wa Barabara na mkandarasi kuhakikisha wanamalizia vipande vya Barabara vilivyobaki kutoka Sale hadi Mto wa Mbu.
Ameyasema hayo alipokuwa akikagua mradi wa Barabara ya Waso hadi Sale Wilayani Ngorongoro.
Serikali imeshatoa zaidi ya shilingi Bilioni 42 mpaka sasa ili ziweze kumaliza kipande cha Barabara kutoka Waso hadi Sale, hivyo amemtaka Mkandarasi huyo kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo Oktoba mwaka huu.
Nae, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amesema Serikali itatangaza tenda kwa vipande vya Barabara hiyo vilivyobaki mapema na kwa awamu ili kurahisisha ukamilikaji wa Barabara hiyo mapema.
Mongella amesema kukamilika kwa Barabara hiyo kutafungua fursa nyingi za kiuchumi katika Wilaya hiyo na hata pia kupunguza muda wa kusafiri.
Pia, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Raymond Mangwala amesema Barabara hiyo ni kama lango la kukuza uchumi wa Wilaya hiyo kwani mwingiliano utaongezea pindi itakapokamilika.
Ameomba ili mradi wa Barabara hiyo uweze kukamilika kwa wakati basi Mkandarasi aliyepo apatiwe tena tenda yakumalizia vipande vya Barabara hiyo kwani tayari anavifaa katika eneo hilo kuliko kupatiwa Mkandarasi mwingine ambae itamlazimu kuleta vifaa katika eneo la mradi ambayo ni gharama.
Ziara ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na Mkuu wa Mkoa ilikuwa na lengo la kukagua Miradi ya kimkakati katika Wilaya ya Ngorongoro ambapo walikagua Barabara ya Waso hadi Sale yenye urefu wa Kilomita 49, Hospitali ya Wilaya, Chuo cha Uwalimu Ngorongoro.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.