Na Elinipa Lupembe
Jumla ya shilingi Bilioni 2.5 zimegawiwa na Serikali kwa kaya 59,904 mkoa wa Arusha, kupitia programu ya Mpango wa
Kunusuru Kaya ya Masikini, mradi unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF III OPEC IV.
Kiasi hicho cha fedha kimegawiwa kwa kaya 62,667 zilizo kwenye mpango, kwenye vijiji/mitaa 577 vya halmashauri zote saba za mkoa wa Arusha, ikiwa ni uhawilishaji fedha kwa dirisha la miezi miwili ya Novemba na Desemba mwaka 2023.
Akizungumza na mwandishi wetu, Mratibu wa TASAF Mkoa wa Arusha, Richard Nkini, amesema kuwa, mgawanyo huo wa fedha umezingatia kaya zilizo kwenye mpango kwa kila halmashauri, na kuutaja mgawanyo kuwa, kiasi cha shilingi milioni 551.6 zimegawiwa kwa kaya 13,795 za halmasahuri ya Arusha, shilingi milioni 174.6 kwa kaya 4,385 za halmashauri ya Jiji la Arusha na shilingi milioni 328.9 kwa kaya 7,761 za halmashauri ya Karatu.
Shilingi milioni 318 kwa kaya 7,177 halmashauri ya Monduli, shilingi milioni 447.1 kwa kaya 10,111 halmashauri ya Ngorongoro, milioni 301.6 kwa kaya 7,769 halmashauri ya Meru huku shilingi milioni 388.9 zikigawiwa kwa kaya 8,905 za halmashauri ya Longido.
Mratibu huyo ameeleza kuwa, lengo la Serikali la kuhawilisha fedha hizo ni pamoja na kuziwezesha kaya hizo kujiinua kiuchumi na kijamii, kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF pamoja mradi wa kuweka akiba kupitia vikundi vya kuweka, kuwekeza na kukopa.
Aidha, amefafanua kuwa, TASAF ni mpango wa serikali unaolenga kusaidia kaya masikini nchini, kupitia uhawilishaji fedha moja kwa moja kwa walengwa, ili kuinua hali ya maisha ya kaya zilizo katika mazingira hatarishi na kuhakikisha kaya hizo zinatumia fedha hizo kulingana na ruzuku zilizoainishwa za msingi, elimu na afya
"Mpango wa TASAF ni jitihada za Serikali za kupunguza umaskini na kukuza maendeleo ya jamii, kupitia programu ya kutoa fedha moja kwa moja kwa walengwa ili kuongeza upatikanaji wa huduma za msingi kama elimu na afya, na kuboresha uwezo wa kaya hizo kujikimu kiuchumi
Programu hiyo imekuwa na matokeo chanya kwa walengwa katika kupunguza umaskini uliokithiri na kuongeza ustawi wa jamii nchini kupitia tathmini ambayo hufanywa kwa kina na kuhakikisha kuwa misaada inawafikia walengwa kwa usahihi.
#arushafursalukuki
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.