Na Daniel Gitaro
Chuo kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimetakiwa kuwekeza zaidi kwenye teknolojia ya kisasa, katika utoaji wa elimu ili kuendana na kasi ya ulimwengu wa sasa ambao umejikita zaidi kwenye mifumo ya kiteknolojia.
Rai hiyo, imetolewa na Mkuu wilaya ya Arusha Mhe. Felician Mtahengerwa, wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella, wakati wa mahafali ya 42 ya chuo hicho, yalifanyika kwenye viwanja vya chuo hicho Kampasi ya Mkoa wa Arusha.
Mhe. Mtahengerwa, amesema kuwa, kutokana na maendeleo ya Sayansi na teknolojia, uongozi wa chuo hicho, kuwekeza kwenye teknolojia ya kisasa ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia ya kisayansi.
Aidha, licha ya kuupongeza uongozi wa chuo hicho kwa elimu wanayoitoa sambamba na wahitimu katika kada mbalimbali, amewataka wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kuleta mabadiliko chanya katika maeneo yao ya kazi pamoja na kuchochea jitihada za kuleta maendeleo na mapinduzi katika Nchi yetu.
"Nendeni mkaitumie elimu hii mliyoipata hapa kuleta mapinduzi makubwa ya kimaendeleo katika sehemu zenu za kazi na kuleta mabadiliko kwenye jamii na Watanzania wote kwa ujumla". Amesisitiza.
Akisoma risala ya wahitimu, mhitumu wa shahada ya uzamili kitivo cha maktaba na usimamizi wa habari, Rafiki Kilonzo amebainisha kuwa chuo hicho kimekuwa ni fursa kwa wanafunzi kujiendeleza katika ngazi zote za elimu na kuwawezesha wahitimu kufikia malengo yao kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Ameongeza kuwa, licha ya mchango mkubwa unaotolewa na chuo hicho, bado kinakabiliwa na changamoto kadha wa kadha ikiwemo baadhi ya wanafunzi kutokuwa na miundombinu rafiki kama vile teknolojia ya TEHAMA, habari na mawasiliano pamoja na uchumu mdogo unaopelekea baadhi kushindwa kumaliza masomo yao kwa wakati.
"Tunaomba viongozi wa Sekta ya walimu wazidi kutoa ushirikiano kwa walimu kwa kuweka mazingira wezeshi zaidi kwa walimu wakati wa mafunzo ya vitendo ili elimu hii iweze kuwafikia na vijana wenzetu popote walipo". Amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa chuo hicho, Dkt. Nangwale Msofe amesema kuwa chuo hicho kimeongeza fursa ya upatikanaji wa elimu Mkoani Arusha kwani tangu kuanzishwa kwake kimehudumia wanafunzi zaidi ya 7500.
Aidha ametumia fursa hiyo kuipongeza na kuishuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwezesha mradi wa Hit project ambao umewezesha wanafunzi 300 kusoma nje ya nchi kwa mwaka wa masomo 2021/2022 jambo ambalo limechagiza ongezeko la udahili wa wanafunzi kituoni hapo.
"Tunamshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia mradi huo unaosimamiwa na Benki kuu ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu wenye madhumuni ya kutengeneza na kung'arisha mazingira ya ufundishaji kwa elimu ya juu na kufadhili ujenzi wa maabara ya sayansi na ofisi ya kituo cha Arusha". Amesema Mkurugenzi huyo.
Awali, jumla ya wanafunzi 241 wamehitimu masomo yao kwa ngazi tofauti tofauti ikiwemo shahada ya uzamivu (phd), shahada ya uzamili, shahada ya kwanza, stashahada pamoja na astashahada.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.