Na Mwandishi wetu - Meru DC
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Amir Mohamed Mkalipa ametoa pongezi na shukrani kwa Shirika lisilo la kiserikali la "Cross Talent Share International"(CTSI) kwa msaada wa vifaa vyenye thamani ya shilingi Milioni 24.9 katika shule ya Sekondari ya King'ori iliyopata majanga ya kuunguliwa na Bweni la Wasichana.
Mhe. Mkalipa ametoa shukrani hizo mara baada ya kupokea vifaa hivyo Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Meru na kuvipeleka moja kwa moja katika shule ya Sekondari Kin'gori iliyopo Kata ya Malula.
"Kwa niaba ya Serikali tunawapongeza wenzetu wa CTS International kwani taasisi hii imekuwa ikisaidiana na Serikali kuhakikisha inatoa msaada kwa watoto wetu waliopatwa na majanga ya moto" amesema Mkalipa.
Aidha, Mkuu wa Wilaya Mkalipa ameeleza kuwa Serikali inajenga majengo kwa gharama kubwa hivyo amewataka viongozi wa Kata, Mkuu wa Shule na Jamii kutoa wito kwa wanafunzi, wazazi na jamii nzima kuilinda miundombinu hiyo kwani ni ya gharama kubwa.
Mwakilishi wa shirika la CTSI Bw. Justin Mwaisemba ameeleza kuwa CTSI ilitoa msaada wa vitu vyenye thamani ya sh.Mil 5.5 baada ya kupata majanga ya kuunguliwa na Bweni la wasichana na kuahidi kutoa vifaa vya ukarabati wa jengo lililoungua hivyo wamekuja kutimiza ahadi.
"Leo tumekuja kutekeleza ahadi tuliyoitoa Julai Mosi 2024 ya kuleta vifaa vya ukarabati vyenye thamani ya Shilingi Milioni 24.9. Tumeleta Mbao, Mabati, Madirisha, Mifuko Ya simenti, ndoo za rangi, Gypsum board na vifaa vingine vyote." amesema Mwaisemba .
Mkuu wa shule ya Sekondari Kin'gori Mwl. Justiwin N. Mutungi ametoa shukrani za dhati kwa niaba ya wanafunzi wa shule hiyo kwa taasisi ya CTSI na Serikali kwa msaada waliopata kwani msaada huo utaleta tija na kuwafanya wanafunzi hao kuendelea vyema katika katika masomo yao.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Meru Mwl. Zainabu J. Makwinya ametoa shukrani kwa Shirika la CTSI kwani kwa msaada waliotoa imesaidia kuipungizia Serikali jukumu kwani Halmashauri pekee isingeweza kukarabati jengo hilo kwa haraka .
Bweni lililoungua na Mōto nililikuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 68.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.