Aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Monduli Mhe. Joshua Nasari, amepata fursa ya kuagana rasmi na viongozi na watumishi wa mkoa wa Arusha, mara baada ya kuhamishwa na Rais Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kutoka wilaya ya Monduli na kwenda kuwa Mkuu wilaya ya Magu, mkoani Mwanza.
Mhe. Nasari amepata fursa ya kuaga wakati wa hafla fupi ya kumuapisha Mkuu mpya wa wilaya ya Monduli Mhe. Festo Shemu Kiswaga, iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha.
Hata hivyo, Mhe.Nasari amesema kuwa ameondoka Monduli, huku akijivunia mafanikio makubwa aliyoyaacha wilayani hapo, akilinganisha na hali mbaya aliyoikuta, ikiwepo ongezeko la ukusanyaji wa mapato, utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na utoaji na upatikanaji wa huduma za jamii pamoja na utatuzi wa kero za wananchi.
Aidha, amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumuamini kuhudumu kwenye Serikali yake ya Awamu ya sita na kuendelea kuwahudumia watanzania hususani wananchi wa wilaya ya Magu na kuahidi kuongeza kasi zaidi ya kufanya kazi.
"Ninamshukuru Dkt.Samia Suluhu Hassan,kwa kuniamini, uhamisho huu umenipa funzo kuwa utumishi wa Umma ni popote, ninaahidi kuendelea kuchapa kazi ikiwa ndio mkakati wa kuwahudumia wananchi na kufikia malengo ya Serikali".Amesema Mhe. Nasari
Awali, Viongozi, Watumishi na Wananchi wote wa mkoa wa Arusha, wamemtakia kila la kheri Mhe.Nassari kwenye kituo chake kipya cha kazi na kumtaka kuendeleza mazuri na mema aliyoyafanya Monduli kwa kufanya kazi kwa bidii ya kulitumikia Taifa katika wilaya ya Magu kwa maendeleo ya watanzania.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.