Na Daniel Gitaro
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini imetoa mafunzo kwa Asasi za kiraia zinazotoa huduma kwa waraibu wa Dawa za Kulevya juu ya uandishi mzuri wa maandiko ya miradi itakayowawezesha kudhibiti matumizi ya dawa hizo nchini.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Misaile Albano Mussa, Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Uzalishaji Mali, Hargeney Chitukuro amesema kuwa, mafunzo hayo ni muhimu kwa Asasi hizo ili kutoa elimu zaidi na matibabu kwa waraibu wa dawa za kulevya sambamba na umakini wa matumizi ya fedha kwaaajili ya utekelezaji wa kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Ameongeza kuwa, uandikaji wa maandiko ya miradi ni muhimu yakazingatiwa ili kusaidia Serikali katika mapambano ya matumizi ya dawa hizo za kulevya sanjari na udhibiti wake kwa kuibua miradi mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kwa Jamii kuanzia shuleni, vyuoni, Taasisi za fedha na n.k.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii ofisi ya DCEA Kanda ya Kaskazini, Sarah Ndaba amesema elimu hiyo ya uandishi wa maandiko ni muhimu kwani itasaidia wadau hao katika kusaidia Jamii kupata elimu pamoja na ufanyaji kazi kwa ufanisi zaidi na kuisaidia Serikali kwenye mapambano hayo.
Vileile amsema kuwa, mamlaka hiyo ina jumla ya Asasi zaidi ya 100 na kwa Kanda ya Kaskazini wanashirikiana na Asasi zaidi ya 16 ambazo zinatoa mrejesho juu ya udhibiti wa dawa hizo pamoja na utoaji mrejesho kwa mamlaka ya DCEA juu ya mchanganuo wa kazi walizofanya na watakazofanya kwa kila mwaka.
"Lazima kuwe na weledi katika uandishi wa maandiko yao ili kupata uelewa na mbinu mpya ya maandiko bora ya kushawishi wafadhili kutoa fedha kwaaajili ya mapambano hayo nchini kwani Asasi za kiraia zina umuhimu mkubwa wa kupambana na dawa hizo ikiwemo utoaji elimu kwa jamii". Amesema.
Naye mmoja kati ya washiriki wa mafunzo hayo kutoka Shirika la Gift of Hope Foundation ,la Mkoani Tanga, Said Bandawe amesema mafunzo hayo ni muhimu kwao kwani yatawasaidia kupata fedha sanjari na kufanya harambee ili kukusanya fedha kwaaajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za kudhibiti dawa hizo ikiwemo utoaji wa elimu kwa jamii zote.
Wakati huo huo, Afisa Elimu wa Mamlaka hiyo (DCEA), Shabani Miraji ameongeza kuwa mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali nchini ili kudhibiti dawa hizo sambamba na utoaji elimu zaidi na kubaini mbinu mpya wanazotumia wafanyabiashara wa dawa hizo na jinsi ya kuwadhibiti.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.