Naibu Katibu Mkuu anayeshughilikia Afya Ofisi ya Rais - TAMISEMI Dkt. Charles Mahera amewataka wadau kuangalia uwezekano wa kuongeza ufadhili wa kuwezesha mfumo wa usamizi wa huduma za Afya kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa (GOTHOMIS) kuunganishwa kwenye vituo vya kutolea huduma kwenye Mikoa 25 iliyobakia.
Dkt. Mahera ametoa ombi hilo wakati wa ziara ya ujumbe kutoka Ubalozi wa Korea ya Kusini nchini Tanzania wenye lengo la kuona maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Kupanua matumizi ya GOTHOMIS mkoani Dodoma.
Amesema mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Korea ya Kusini kupitia shirika lake la Ushirikiano wa Kimataifa (KOICA) unatarajia kuvifikia vituo 235 vya kutolea huduma za afya mkoani Dodoma.
Aidha amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo umeleta tija kwa vituo vinavyotumia mfumo huo hivyo amewaomba KOICA kupitia ubalozi wa Korea ya Kusini kuangalia uwezekano wa kuwezesha mradi huu kufika katika Mikoa mingine ili kuongeza uimarishaji wa matumizi ya Mfumo wa GOTHOMIS katika utoaji wa huduma za afya.
Naye kaimu Balozi wa Korea ya Kusini nchini Tanzania Ndg. Seung Yeon Lee alisema amefurahishwa na utekelezaji wa mradi na hatua zilizofikiwa licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa.
Ujumbe huu kutoka Ubalozi wa Korea ya Kusini pamoja na kutembelea Ofisi ya Rais - TAMISEMI, ulitembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma pamoja na kutembelea kituo cha Afya Makole ambacho kimekamilisha mafunzo na kuanza matumizi ya mfumo wa GOTHOMIS chini ya ufadhili wa mradi huo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.