UCHUMI WA ARUSHA
Unapogusa uchumi wa mkoa wa Arusha hususani jiji la Arusha na mzunguko wake wa fedha kwa asili yake, moja kwa moja chanzo chake kikuu ni sekta tatu ambazo ni Mikutano, Madini na Utalii.
Katika historia ya Tanzania ,Arusha katika diplomasia ya uchumi inasimama kama kinara wa Diplomasia ya Utalii wa Mikutano, Matukio na Maonyesho.
Tukiangazia eneo la mikutano, kwa miaka zaidi ya 40 sasa mnyororo wa thamani wa mikutano umekuwa mkubwa kwa kutengeneza ajira na kipato.
Mnyororo huo wa thamani wa mikutano umegusa makundi mbalimbali yakiwemo ya mahoteli, utalii, wenye vyombo vya usafiri, wakulima wa mbogamboga na matunda pamoja na wenye mabaa, maeneo ya burudani na starehe na hata wenye maduka.
MTENDAJI MKUU WA AICC
Mwamba wa Kaskazini Edward Ngoyai Lowassa aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha(AICC) Mwezi Disemba 1989.
Alishikilia nafasi hiyo hadi mwezi Disemba 1990. Alikuwa Mtendaji Mkuu wa Kituo hicho wa tatu akitanguliwa na Frank Mwanjisi(Julai 1978 hadi Machi 1980) na Sammy Mdee (April 1980 hadi Agosti 1989)
AICC ilianza mwaka 1978 huku sehemu kubwa ya shughuli zake zikifanyikia katika mali zilizoachwa baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki(EAC) ya awali mwaka 1977.
Mali hizo ni pamoja na jengo kubwa la makao makuu likiwa na ukumbi mkubwa na maarufu wa Simba na baadaye zikabuniwa kumbi zingine za mikutano,maofisi ya kupangisha, nyumba za kupangisha zaidi ya 600 na hospitali.
CHANGAMOTO YA BIASHARA YA MIKUTANO
Mwamba Lowassa alishika nafasi katika kipindi cha kuelekea mabadiliko makubwa ya sera za uchumi, kisiasa na kijamii
Ni kipindi kilichojaa misukosuko katika uchumi wa dunia na wimbi la mageuzi lilikuwa limetanda kwa nchi za kijamaa yaani kambi ya ushoshalisti ilikuwa imedhoofishwa baada ya kusambaratika kwa himaya ya muungano wa Kisovieti(USSR) na washirika wake wa ulaya ya mashariki.
Mabadiliko hayo yalileta sura mpya katika medani ya uhusiano na ushirikiano wa kimataifa.
Chama cha Mapinduzi(CCM) kililazimika kuzifanyia mabadiliko sera zake uchumi za miaka ya tisini kwa kufanya uchambuzi wa programu ya chama ya mwaka 1987 hadi 2002
Ndani ya nchi, taifa lilianza kutekeleza sera za mageuzi ya kiuchumi baada ya kufikia makubaliano na Benki ya Dunia(WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa(IMF)
Mageuzi hayo ni pamoja na kuongeza ufanisi katika mashirika ya umma na kuipunguzia mzigo serikali wa kutoa ruzuku ya kuendesha mashirika hayo.
Mashirika yalibinafsisha na mengine kuingia ubia na makampuni binafsi huku mashirika ya umma ambayo yaliendeshwa kwa ufanisi yaliendelea kuwa ya serikali.
MPANGO MKAKATI WA LOWASSA
Mwamba Lowassa aliingia katika kipindi hicho akitokea Makao Makuu wa Chama cha Mapinduzi(CCM) kama ofisa wa chama hicho Dodoma.
Mwamba aliingia AICC ikiwa katika maarifa kongwe na teknolojia duni huku akitambua suluhisho pekee ni kujenga misingi ya uendeshaji wa kisasa kwa kuwekeza katika kukuza maarifa ya wafanyakazi na kuingiza teknolojia ya kisasa katika utoaji wa huduma na uendeshaji.
katika kipindi cha mwaka mmoja aliokaa AICC kama Mkurugenzi Mwendeshaji, Mwamba Lowassa aliweza kukarabati na kupaka rangi mamia ya nyumba zote za shirika hilo pamoja na kuboresha mazingira yaliyokuwa yameachwa yakizorota kwa miongo mingi.
Mwamba alifanya ukarabati wa kumbi zote za mikutano na kufunga vifaa vya kisasa kwa mikutano.
Ama katika eneo la masoko, Mwamba alisimamia utengenezaji wa filamu ya kimataifa kupitia kampuni maarufu duniani, Camerapix ya marehemu Mohamed Amin iliyotangaza AICC na vivutio vya utalii na mbuga za wanyama pamoja na mahoteli yote ili kuvutia mikutano ya kimataifa.
Kwa filamu Iliyojumuisha hifadhi za taifa na kumbi za mikutano hiyo inaweza kuwa kama vile filamu ya 'The Royal Tour' .
Licha ya filamu pia Mwamba alitumia mkakati wa kwenda kuitafuta na kuichononoa mikutano ya kimataifa ambayo ni muhimu kwa kuingiza fedha za kigeni kutokea huko kwenye chanzo chake.
Mikutano hiyo ni pamoja na inayohusu kilimo katika Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO) huko Roma,mikutano ya elimu katika Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO) huko Paris pamoja na mikutano mingine inayoanzia Jumuiya ya Ulaya(EC) huko Brussels, Muungano wa Nchi za Afrika(OAU) huko Addis Ababa na Umoja wa Mataiga,(UN) huko Geneva, Nairobi na New York,
Mwamba Lowassa aliboresha utawala wa AICC kwa kuajiri vijana wasomi na mabingwa katika idara zote, hasa za masoko, fedha, miliki ya nyumba na hospitali.
LOWASSA KATIKA MICHEZO
Katika nyanja za michezo, Mwamba alivifanyia ukarabati viwanja vyote vya michezo.
Michezo hiyo ni pamoja na mpira wa miguu, netiboli, volleyball, tennisi, squash na basketball kwa ajili ya wageni na jumuiya ya watu wa Arusha.
Aidha Mwamba Lowassa alihamasisha na kuwezesha timu ya netiboli ya AICC mpaka ikawa bingwa wa taifa wa mchezo huo.
WAANDISHI WA HABARI ARUSHA
Mwamba Lowassa katika mkakati wa kukitangaza zaidi AICC alitambua mchango wa Wanahabari hiyo alisaidia sana kuimarika kwa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha(APC)
APC kilikuwa miongoni vya vyama vya awali kabisa cha waandishi wa mikoa kuundwa.Ilianzishwa mwishoni mwa miaka ya 1980.
Lowassa alitoa ofisi ya bure katika jengo la AICC pamoja na samani za ofisi.
BURIANI MWAMBA WA KASKAZINI EDWARD NGOYAI LOWASSA
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.