Mkurugenzi wa Idara ya Vijana bwana James Kajuguzi,amesema Ofisi ya Waziri Mkuu imatenga kiasi cha shilingi bilioni 5 zitakazo wawezesha vijana kupata ujuzi wa kutengeneza Kitalu Nyumba na elimu ya Kilimo katika vitalu hivyo.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi pamoja na kamati ya mikopo ya vijana ya Jiji la Arusha kwa lengo la kukagua maendeleo ya mikopo inayotelewa kwa vijana na hali nzima ya urejeshaji wa mikopo hiyo.
“Hizi bilioni 5 zitaenda kutoa elimu kwa vijana 20 kwa kila Mkoa juu ya utengenezaji wa Vitalu Nyumba na vijana wengine 80 watapatiwa mafunzo ya kilimo bora cha vitalu nyumba”.
Amesisitiza zaidi kuwa baada ya mafunzo hayo Wizara imetenga kiasi cha bilioni 1 kwa ajili ya mtaji kwa hao vijana watakaopenda kwenda kujiajiri kwenye kilimo cha biashara cha Kitalu Nyumba.
Kajugusi amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu imekuja na mpango huo wakutoa elimu ya kutosha kwa vijana juu ya kilimo cha biashara kwa kutumia Kitalu Nyumba ili kuongeza wigo mkubwa kwa vijana kupata fursa za uzalishaji na kuinua uchumi wao.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya mikopo kwa Jiji la Arusha Afisa Maendeleo ya Jamii Hanifa Ramadhani, amesema kwa jiji la Arusha mwaka 2008/2009 Wizara ilitoa kiasi cha fedha Milioni 10 na zilisharejeshwa.
Mwaka 2016/2017 pia Jiji walipatiwa kiasi cha fedha shilingi Milioni 20 na marejesho yake yanaendelea.Pia katika mikopo ya Halmshauri ya asilimia 4 kwa vijana, mwaka 2018/2019 walitoa kiasi cha milioni 665 kwa vikundi 118 na asilimia 2 ya walemavu wametoa kiasi cha milioni 25 kwa vikundi 5.
Mkurugenzi wa Kampuni ya KCG Investment Glory Wilfred amesema, mikopo wanayopatiwa na serikali kweli imesaidia kuinua mtaji wao na kuwafanya waendelee kuzalisha zaidi bidhaa zao.
Amewashauri vijana wengine kujiunga katika vikundi ili waweze kupatiwa mikopo ya kuwainua kiuchumi na amewataka wawe waaminifu katika kurudisha fedha hizo ili ziwasaidie wao kwa kukopa tena au kutoa fursa na kwa vijana wengine kukopeshwa.
Kajugusi anaendelea na ziara yake katika Halmashauri za Mkoa wa Arusha ili kukagua maendeleo ya mikopo ya vijana na hali ya urejeshaji wake.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.