Waratibu wa lishe ngazi ya Mkoa na Halmshauri Mkoani Arusha wametakiwa kwenda kutoa elimu ya lishe katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye nyumba za Ibada, mashuleni,minadani na kwenye kamati za lishe za Kata.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella alipokuwa akizungumza na Kamati ya lishe Mkoa wakati wa kikao kazi cha tathimini ya lishe ngazi ya Mkoa.
Mongella amesema kuwa tathimini inayofanyika katika viashiria vya lishe haitoshi kujitathimini na kujihakikishia kuwa elimu ya lishe inayotolewa imewafikia wananchi kwa kiwango kikubwa,bali mikakati madhubuti inatakiwa ijengwe mpaka kwenye Kaya kwa kuhakikisha kila mzazi ananatambua umuhimu wa lishe kwa familia.
Katika kusisitiza hilo amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kwenda kusimamia agenda ya lishe kwa umakini ikiwemo kuhakikisha vikao katika ngazi zao vinafanyika kwa wakati na Wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu faida ya lishe wa Jamii.
"Ndugu zangu suala la lishe tusifanye nalo mchezo, lina mchango mkubwa sana katika maendeleo ya Nchi,lishe bora ndiyo inayochangia ustawi wa afya ya mwili na akili kwa watu wetu kwani ndipo wanapopatikana wataalamu mbalimbali katika sekta zote." Alisema Mongella
Akichangia mjadala huo,Katibu Tawala wa Wilaya ya Arumeru James Chembe amesema katika kushughulikia suala la lishe ni vyema wataalamu kama maafisa Kilimo na Mifugo wakashirikishwa kwenye mpango kazi kwani kada zao zina mchango mkubwa katika masuala ya lishe bora.
"Hapo zamani tulikuwa tuna utaratibu kwa kila Kaya kuwa na bustani za mbogamboga na kuwa Mifugo ambayo ilisaidia upatikanaji wa vyakula vya lishe na maziwa,nashauri kurudishwe utaratibu wa kulima bustani katika shule zetu ili wanafunzi waweze kupata chakula bora wakiwa majumbani na shuleni.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Arusha, Sulemani Msumi amesema kuna haja ya kutungwa sheria itakayowabana wazazi ambao watakaidi kuchangia fedha za chakula katika shule ili wanafunzi waweze kupata chakula cha mchana kwani hii itasaidia kupunguza wimbi la watoto wengi kukosa chakula shuleni.
Kikao cha Tathimini ya afua za lishe ngazi ya Mkoa kimejumuisha robo ya kwanza naya pili katika mwaka wa fedha 2022/2023.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.