Mkuu wa Mkoa wa Arusha Iddi Hassan Kimanta, amesema atasimamia uundwaji wa mabaraza ya wazee katika wilaya za Mkoa wa Arusha ambazo bado hazijaunda.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wazee katika mkutano wa hadhara wilayani Karatu, ikiwa ni maadhimisho ya siku ya wazee duniani.
Kimanta amesisitiza kuwa wazee ni hazina kubwa katika ujenzi wa nchi,hivyo changamoto zao atahakikisha anazisimamia kwa umakini na ataanza kuboresha huduma zao za afya na kuhakikisha kila mzee anapata kitambulisho cha utambuzi.
Akisoma risala kwa niaba ya wazee kwa Mkuu wa Mkoa, Katibu wa baraza la ushauri la wazee Mkoa, bwana Hamis Ramadhani amesema,katika huduma za afya kuna baadhi ya vituo vya afya wanazingatia sera ya mzee kwanza lakini kuna baadhi ya maeneo hawazingatii.
Aidha, wameiyomba serikali kuwapatia mikopo katika vikundi vidogo vya wajasiriamali kama ilivyo kwa wamama, vijana na wenye ulemavu ili iwasaidie katika kujikwamua kiuchumi.
Nae, afisa maendeleo ya jamii bwana Denis Mgiye amesema, jumla ya wazee 67497 kwa Mkoa mzima wameshatambuliwa na kupewa vitambulisho.
Amesema Mkoa unaendelea kuhakikisha changamoto mbalimbali za wazee zinatatuliwa ikiwemo; wamesimamia uundwaji wa baraza la ushauri la wazee ngazi ya Mkoa na lina jumla ya wazee 49 lenye wajumbe kutoka kila Wilaya.
Mkoa umetoa ofisi kwa baraza hilo la wazee Mkoa ili waweze kuendesha shughuli zao.
Maadhimisho ya siku ya wazee Duniai hufanyika kila mwaka Octoba mosi na kwa mwaka huu 2020 Kimkoa maadhimisho haya yamefanyika Wilayani Karatu, yenye kauli mbiu isemayo “Familia na Jamii, tuwajibike kuwatunza wazee”.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.