Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru imefanya Mkutano wa kwanza na Jumuiya ya wachangiaji wa damu wa kudumu wanaojulikana kama Mount Meru Blood Donation Family iliyoanzishwa Januari 18, 2023 katika hospitali ya Mount Meru.
Akifungua Mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella ameeleza kuwa kupitia zoezi la uchangishaji wa damu
Unaoendelea, Mkoa wa Arusha umeweka rekodi wakutokuwa na uhaba wa damu na ameupongeza Uongozi wa Mount Meru kwa ubunifu wa maono yenye tija katika kutafuta suluhisho la tatizo la uhaba wa damu katika hospitali ya Mkoa wa Arusha na Mikoa jirani kwa kuunda Jumuiya ya wachangiaji damu wa kudumu wanaotambulika na hospitali.
Mhe. Mongella amewaasa wanajumuiya hao kuendelea kuhamasisha wananchi wengine kujiunga na familia hiyo ili kuchangia damu ambayo itaenda kuwaokoa Watanzania wengine wenye uhitaji kwani kufanya hivyo ni thawabu kwa Mungu.
"Kuchangia damu ni moyo wa kipekee sana kwasababu damu ni uhai na haipatikani kwa njia nyingine yoyote, hivyo ukitoa uhai kwaajili ya mtu mwingine ni jambo lenye baraka sana kwa Mungu". Amesema.
Akisoma taarifa fupi, Mganga Mfawidhi wa Mount Meru Dkt. Alex Ernest alieleza, dhumuni la kuanzisha Jumuiya hiyo ya wachangiaji wa damu wa hiyari ni kukabiliana na changamoto zitokanazo na uhaba wa Damu na mazao ya Damu katika hospitali ambapo matumizi ya damu yaliongezeka kufikia chupa 500 kwa mwezi kutoka chupa 350 katika mwaka wa fedha 2020/2021 hali iliyopelekea kuwa na upungufu wa damu na kusababisha ucheleweshwaji wa huduma za matibabu.
Familia hiyo ya Wachangiaji wa Damu wamepewa kadi maalumu za uchangiaji wa damu wa kudumu na watapata kipaumbele kwenye huduma za afya kama vile punguzo kwenye huduma ya malazi kwa wodi binafsi, kupata huduma za haraka za matibabu (fast track services) na kupata huduma za kuongezewa damu pindi watakapokuwa na uhitaji huo na hii ni njia yakuleta hamasa na kuongeza wigo wa uchangiaji wa damu na hadi sasa jumla ya chupa 10781 za damu zimefanikiwa kukusanywa kwa kipindi cha mwaka mmoja toka Mount Meru blood donation family kuanzishwa.
Hata hivyo, baadhi ya wanajumuiya hao wamesema kuwa, lengo kubwa la kujiunga na familia hiyo ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha huduma za Afya Nchini na kupunguza gharama kubwa za matibabu pamoja na vifo kwa wananchi.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.