Kama ambavyo amekuwa akisema mara zote Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda kuwa kila anachokifanya Mkoani hapa anatamani kiwe na tija kwa wakazi wa Arusha, ndivyo ilivyo kwa Mussa Moto, mmiliki wa Motoland Garage wanaojishughulisha na utengenezaji wa magari chapa ya Land Rover.
Ujio wa Land Rover Festival 2024 Jijini Arusha itakayofanyika Oktoba 12- 14, 2024 kumeongeza biashara kwa Mussa ambaye anakiri wazi kuwa zipo gari nyingi aina ya Land Rover ambazo zimeletwa kwake zikitakiwa kurekebishwa haraka, tayari kushiriki kwenye Land Rover Festival 2024.
"Tunashukuru ujio wa Land Rover Festival kwenye Jiji letu la Arusha kwasababu itatuletea mafundi kupata ajira zaidi kwasababu wateja wengi wapo mbali na tamasha hili litatuletea wateja pamoja, tunashukuru kwa Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Makonda kuweza kutufikiria na kutuletea jambo hili sisi wananchi wa chini tunaamini utapata fursa ya kutangaza ubunifu wetu."Amesema Bw. Mussa.
Mussa Moto ni miongoni mwa mafundi wa mwanzo kabisa Jijini Arusha ambao tangu mwaka 2009 yeye na wasaidizi wake wamekuwa wakishughulika na kubadilisha mionekano ya magari ya Land Rover za zamani kuzileta kwenye muonekano wa Kisasa.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.