"Zoezi la kuwapanga Machinga katika Mkoa wa Arusha litafanyika kwa utulivu na litakuwa shirikishi kati ya viongozi wa Serikali na Viongozi wa machinga wenyewe."
Yamesemwa hayo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, Jijini Arusha.
Amesema zoezi hilo ni maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan hivyo yeye kama msimamizi wa Mkoa huo atahakikisha linakuwa shirikishi kwa pande zote.
Amesisitiza pia,wamachinga ni watanzania na wanahaki yakuhudumiwa kama watanzania wengine hivyo zoezi litakuwa la haki.
Amewataka wananchi wote wa Mkoa wa Arusha kutokuwa na taharuki yoyote kwani waiamini Serikali yao na hasa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwani mpango ni mzuri kwa ujenzi wa Taifa letu.
Viongozi wa Mkoa wa Arusha watashirikiana na wananchi hasa wamachinga, wafanyabiashara wakubwa, wakati na wadogo ili kujenga uchumi wa Mkoa kwa pamoja.
Amesema asitokee mtu akabeza au kuvuruga utaratibu utakaowekwa baada ya maamuzi kufanyika kwani Serikali ya awamu ya sita anawajali wananchi wake kwa kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya biashara, hivyo atadhibitiwa vikali.
RC Mongella ametoa ufafanuzi huo ikiwa ni maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan baada ya kuwaapisha mawaziri wapya mapema jana Jijini Dodoma.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.