Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Bwana Missaile Musa amewataka wadau wa lishe Mkoani humo kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha sekta hiyo inaeleweka katika jamii.
Ameyazungumza hayo katika kikao cha kamati ya lishe Mkoa katika robo ya tatu ya mwaka 2022/2023.
Swala la lishe ni mtambuka hivyo kila mtu ahakikishe anasimama katika nafasi yake kwa kuhakikisha elimu inawafikia watu wote.
Aidha, amewataka wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha maji yanafika katika shule zote za Mkoa wa Arusha ili wanafunzi waweze kupata maji safi na salama.
"Kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko kwa watoto",alisema Missaile.
Pia, amezitaka Halmshauri za Mkoa wa Arusha kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vibao vya kupimia urefu watoto hii itasaidia kupunguza zaidi hali ya udumavu.
Bwana Missaile amesema hali ya udumavu katika Mkoa imeshuka kutoka 36% 2021/2022 hadi 30% 2022/2023, amesema juhudi zipo katika mkoa wetu lakini bado jitihada za makusudi zinaitajika.
Kwa upande wake, afisa elimu watu wazima akizungumza kwa niaba ya afisa elimu Mkoa Emmanuel Maundo amesema changamoto ya upatikanaji wa chakula katika shule ipo kwani kuna baadhi ya wazazi hawatoi mchango wa chakula kwa madai elimu ni bure.
Amesema katika shule za msingi za Serikali 636, shule 502 ndio zinatoa chakula kwa wanafunzi na shule za Sekondari 174 za Serikali zote zinatoa chakula.
Maundo amesisitiza kuwa kupatikana kwa chakula shuleni kumesaidia wanafunzi kupunza utoro, kuongeza ufaulu na nidhamu kwa wanafunzi imeongezeka.
Nae, Afisa Lishe Mkoa Rose Mamuya amesema hali ya upatikanaji wa chakula katika shule vyingi za Mkoa wa Arusha ni nzuri.
Hivyo mikakati aliyonayo ni kuhakikisha vyakula hivyo vinakuwa vyenye virutubisho vya kutosha na njia moja wapo ni kuhamasisha ulimaji wa mbogamboga unafanyika kwenye shule.
Kikao cha kamati ya lishe Mkoa kimefanyika katika robo ya tatu ya mwaka ikiwa ni utaratibu uliopo wa kuhakikisha kikao hicho kinafanyika kwa lengo la kufuatilia hali ya lishe katika Mkoa.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.