Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha Ndugu Juma Hokororo amesema Maonesho ya kimataifa ya Utalii ya Karibu Kili Fair 2024 yamekuwa ni fursa muhimu ya kuwakutanisha na wadau mbalimbali wa utalii katika kuhamasisha zaidi uwekezaji kwenye sekta ya Utalii wilayani Karatu.
Hokororo ametoa kauli hiyo wakati alipotembelea mabanda mbalimbali ya utalii kwenye Viwanja vya Magereza Kisongo leo Juni 09, 2024 akiambatana na Maafisa kadhaa wa Halmashauri hiyo wanaohusika na Utalii, ikiwa ni Kilele cha Maonesho hayo ya Utalii ya Kimataifa.
Hokororo amesema Wilaya ya Karatu inanufaika sana na sekta ya Utalii kutokana na kuwa lango la Utalii wa Arusha kutokana na eneo hilo kuwa njia ya kuelekea kwenye hifadhi za Ngorongoro na Serengeti na hivyo suala la Utalii wamelipa kipaumbele kikubwa katika kuhakikisha dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan inatekelezeka kikamilifu.
"Tangu Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan atengeneze ile filamu ya The Royal Tour tumeona kuanzia mwaka jana Halmashauri ya Wilaya ya Karatu iliweza kupokea wageni wengi sana na hata mapato.Nilifika Karatu mapato ya Service levy yalikuwa Milioni 500 lakini kwa mwaka huu tunategemea kukusanya zaidi ya Bilioni moja kwenye eneo la service levy peke yake." Ameongeza Hokororo.
Akizungumzia tija ya Utalii katika Wilaya hiyo, Mkurugenzi huyo amesema kwa kiasi kikubwa makusanyo yanayotokana na utalii mengi yamekuwa yakielekezwa kwenye maendeleo ya miundombinu na sekta nyingine za kijamii katika kuhakikisha wananchi wananufaika na maendeleo.
Katika hatua nyingine Hokororo amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda kwa kuwa na msukumo mkubwa wa kukuza Utalii Arusha akiahidi kuendelea kushirikiana nae katika kuhakikisha maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan yanatimia kwa mkoa wa Arusha. @halmashauri_ya_karatu @ikulu_mawasiliano @kilifair @hokororojuma
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.