"Nendeni mkafanyie kazi mapendekezo yatakayotolewa kutokana na tafiti ya Oikos na E-MAC ili kuboresha zaidi mfumo mzima wa hedhi salama".
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Emmanuela Kaganda kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa Mkoa katika kufanya tathimini ya mradi wa utafiti wa soko la taulo za Kike.
Amesema tafiti hiyo itasaidia katika kuboresha mazingira ya hedhi salama kwa wasichana na wakinamama.
Mhe.Kaganda amesisitiza zaidi kuwa hedha salama ni agenda ya Kitaifa na mtambuka kwani inahusu jinsia zote.
Hali kadhalika amesema, Serikali katika jitihada zake zakuhakikisha inaweka mazingira salama katika mfumo mzima wa hedhi salama kwa kuboresha miundombinu katika mashule.
Pia amesema katika juhudi hizo bado kuna changamoto ya gharama za vifaa takribani 60% ya wasichana hawawezi kumudu gharama na hii inatokana na tafiti iliyofanywa na NIMRI 2021.
Vilevile 28% ya wasichana hawana elimu yakutosha juu ya matumizi sahihi ya vifaa hivyo.
Amesema kuna umuhimu mkubwa wa kutazama upya mnyororo wa thamani wa vifaa vya hedhi salama ili viweze kupatikana kwa urahisi.
Amesisitiza zaidi utumiaji wa mifumo ya kijamii katika kutoa elimu kwenye jamii ili kurahisisha zoezi nzima la utoaji elimu.
Nae, Afisa Afya na Mazingira kutoka Wizara ya afya Mariam Mashingo amesema juhudi zinazofanywa na Wizara hiyo nikuhakikisha jamii inavunja ukimya kwa wanaume kushirikishwa katika hedhi salama.
Pia, kuhakikisha wasichana na wanawake wanatumia bidhaa salama na zinazopatikana kwa urahisi kwasababu inagusa maswala mazima ya uzazi na afya kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa OIKOS Mary Birdi amesema shirika hilo likisaidiana na E-MAC wamefanya tafiti juu ya hedhi salama nakubaini kuwa wazazi wengi hawazungumzi na watoto wao pindi wanapofikia umri wa kupata hedhi.
Vile vile Upatikanaji wa vifaa vya hedhi bado nichangamoto hususani maeneo ya vijijini, hata pia gharama bado ipo juu kwa watumiaji wengi hawawezi kumudu.
Amesema utafiti wao uliangalia zaidi soko la vifaa lipoje kuanzia utengenezaji hadi kumfikia mtumiaji, kutambua wadau wanashughulika na hedhi salama na pia namna watakavyoweza kutekeleza zoezi zima la hedhi salama.
Mradi wa utafiti wa soko la taulo za kike Tanzania Vijijini ulianza Januari 2023 katika shule za vijijini kwa Wilaya ya Karatu na Longido Mkoani Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.