Leo Tanzania imeandika historia nyingine katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya umeme baada ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe.Dkt.Doto Biteko kuzindua utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme vya kilovoti 400 Chalinze-Pwani na Zuzu-Dodoma.
Mradu huo wa umeme uliozinduliwa utawezesha umeme wote unaozalishwa katika mradi wa kuzalisha umeme wa JNHPP kufika katika maeneo yote ya mikoa iliyopo Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Migodi, Viwanda na kuimarisha biashara ya umeme Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Dkt. Biteko amesema kutekelezwa kwa mradi huo kunatokana na Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali pamoja na miongozo yake ya namna bora ya kutekeleza miradi ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika kwa lengo la kukidhi mahitaji ambayo yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Amesema kuwa kutokana na jitihada hizo zinazofanywa na Rais Samia katika kuendeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme imepelekea Tanzania kuwa kinara barani Afrika katika usambazaji wa umeme kwa wananchi na hii ni kutokana na takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia.
Ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea na jitihada za kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme nchini ambazo zimewezesha kuongeza uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyopo nchini hadi kufikia Megawati 3,169.26 ambapo mahitaji ya juu ya umeme nchini kwa sasa yamefikia Megawati 1,888.72 ambapo mahitaji hayo hayajawahi kufikiwa kutoka nchi ipate Uhuru na hii ikimaanisha kuwa uchumi unazidi kukua kutokana na kuongezeka kwa shughuli za maedeleo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.