Migogoro ya ardhi, changamoto za mirathi, Wananchi kutokulipwa mafao pamoja na mikopo umiza ni changamoto kubwa zaidi zilizojitokeza wakati wa Kliniki maalum ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa mkoa wa Arusha, kliniki iliyofanyika Mei 08-10 mwaka 2024.
Mhe. Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na wasaidizi wake na wanasheria kutoka Chama cha Wanasheria wa Tanganyika TLS walitatua kero na migogoro zaidi ya 200 huku kero nyingine zikitolewa maelekezo ya utatuzi wake kwa vyombo vya Dola pamoja na mamlaka nyingine za Serikali.
Mhe. Mkuu wa Mkoa anasema kliniki hiyo imemsaidia kutambua changamoto zinazowakabili wakazi wa Arusha pamoja na kuanza kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu hasa migogoro ya ardhi kwa kutafiti na kuchukua hatua kwa watu ama mifumo inayozalisha changamoto na kero hizo zinazowaumiza na kuwatesa wananchi.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda pia amenukuliwa akisema Kliniki hiyo imeisaidia serikali kuelewa na kuwafahamu wasaidizi mbalimbali wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na vile ambavyo wanawatumikia wananchi.
Tayari Mhe. Mkuu wa Mkoa ametangaza kuanza kwa ziara yake ya kuwasikiliza wananchi wa wilaya zote za Mkoa wa Arusha, ziara inayotarajiwa kuanza Mei 20 mwaka huu, akiwataka wananchi wenye kero mbalimbali kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano yake ya hadhara kulingana na atakavyopangiwa.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.