Wajumbe wa Kamati ya siasa Mkoa wa Arusha, wameipongeza Serikali kupitia watalamu wasimamizi wa mradi mkubwa wa ujenzi wa shule mpya ya wasichana Longido Samia Suluhu,kijiji cha Orbomba wilaya ya Longido, mradi wa kimkakati, ambao uko kwenye hatua mbalimbali za ujenzi, unaotegemea kugharimu takribani shilingi Bilioni 3 fedha kutoka Serikali Kuu.
Wajumbe hao, wametoa pongezi hizo wakati wa ziara yao ya kawaida ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM, na kujioneo maendeleo ya ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kimkakati, unaotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita.
Akizungumza mara baada ya kukagua na kupokea taarifa ya mradi huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Thomas Ole Sabaya, licha ya kuwapongeza wasimamizi wa mradi huo, ameipongeza na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita, chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo mkubwa, utakao wasaidia watoto wa kike wa jamii ya kimaasai kupata elimu ndani ya maeneo yao.
"Tunaipongeza na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita, kwa kutoa fedha nyingi za kutekeleza mradi huu, shule hii ni zawadi kwa wasichana wa kimaasai, waliokosa fursa ya kupata elimu kwa miongo mingi, mradi huu ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025" Ameweka wazi Mwenyekiti Sabaya.
Aidha, amewaagiza wasimamizi wa mradi huo, kuwasimamia mafundi kuongeza kasi ya ujenzi pamoja na kufanyia kazi marekebisho madogo madogo yaliyosalia ili mradi ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa, zaidi watoto waanze masomo shuleni hapo kama yalivyo makusudio ya Serikali.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella amesema kuwa, kukamilika kwa mradi huo utakuwa msaada mkubwa kwa watoto wa kike, hasa wa jamii ya kimaasai walioshindwa kupata elimu, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mila na desturi za kabila lao, watoto ambao watapewa kipaumbele kufuatia lengo kuu la Serikali la kujenga shule hizo maalum nchini.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Longido Steven Ulaya, amekiri kupokea maelekezo ya kamati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote, huku kipaumbele chao kikiwa ni kukamilisha mradi huo kwa muda uliokusudiwa.
Awali Mradi huo unagharimu kiasi cha fedha shilingi Bilioni 3 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu wa 2024.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.