Mkuu wa Mkoa wa Arusha ametoa Viti mwendo viwili, Bima za afya tatu na Mitaji ya milioni sita kwa kinamama watatu wanaolea watoto wenye ulemavu na wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali mkoani Arusha.
Mhe. Makonda ametoa msaada huo leo wakati akiwa Mjini Arusha kwenye viwanja vya Ngeresero mara baada ya kupata maombi ya msaada huo kutoka kwa Kinamama hao ambapo wamekuwa sehemu ya mamia ya wakazi wa Arusha waliosikilizwa na kutatuliwa kero zao mbalimbali na Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na ofisi yake.
Wazazi wa watoto hao wamemueleza Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda changamoto za watoto wao ambao wengi wao ni watoto yatima huku wakiishi na mama zao ambao wamekuwa wakiishi kwa utegemezi kutokana na kukosa ajira.
"Ni changamoto ambazo zinatokea na ni kama majaribu vile ya dunia, kwahiyo niwaombe msiwatupe watoto. Hii ni mitihani tu ambayo binadamu anapitia kwahiyo naomba msiwatupe watoto. Msifanye hilo kosa.", amesema Mhe. Makonda.
Mkuu wa Mkoa ameendelea na ziara yake kwenye wilaya mbalimbali za Mkoa wa Arusha ambapo amekuwa akisikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi kwenye mikutano yake ya hadhara ikiwemo kero binafsi ambazo nyingi zimekuwa zikihusisha magonjwa na wengi kushindwa kugharamia huduma mbalimbali ikiwemo za matibabu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.