Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongella amesisitiza ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Jiji la Arusha uwe wa ubora na ukamilike kwa wakati.
Ameyasema hayo alipokuwa akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa ya sekondari kwa Jiji hilo ambayo yalipatiwa fedha kutoka Serikalini katika mpango wa Taifa wa mapambano dhidi ya UVIKO 19.
"Napenda kuwapongeza sana viongozi wa Serikali na kisiasa na wananchi wote kwa Jiji hili kwa ushirikiano mliouwonesha hadi kufikia hatua hii ya umaliziaji wa vyumba hivi vya madarasa".
Amewahasa mshikamano huo uendelee katika kuleta maendeleo hata kwenye sekta nyingine.
Katika Jiji la Arusha wamejenga madarasa 105 na 16 niya gorofa na 89 ni majengo ya kawaida.
RC Mongella amesisitiza zaidi kuwa katika shughuli za kuleta maendeleo siasa isiingizwe bali mshikamano uendelee kuwepo.
Aidha, amesema mwisho wa ujenzi wa vyumba vyote vya madarasa kwa Mkoa mzima wa Arusha ni Disemba 10.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt. Onesmo Mandike amesema Halmashauri hiyo ilipatiwa fedha kiasi cha Bilioni 2.1 kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa 105.
Hadi sasa hali ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa Jiji hilo ni mzuri na kasi yake ni nzuri imefikia asilimia 80.
Diwani wa kata ya ungalimitedi bwana Amoor Hussein Omary ameishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha kiasi cha Milioni 80 katika shule ya Sekondari Ungalimitedi.
Amesema kukamilika kwa shule hiyo kutaondoa hadha ya watoto wao kutembea umbali mrefu kwenda shule za mbali kwani hapo awali wazazi walilazimika kutoa nauli ya shilingi 1000 kila siku kwa watoto wao na hiyo ikapelekea ugumu kwa watoto wengi kwenda shuleni.
Ziara ya Mhe.Mongella ya kukagua vyumba vya madarasa ni mwendelezo wa ziara zake katika Mkoa wa Arusha ya kuhakikisha fedha za Serikali Bilioni 8.5 za ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa Mkoa mzima zinatumika kama ilivyopangwa na madarasa yanakamilika kwa wakati.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.