Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa nchi za Afrika wametakiwa kuandaa mapendekezo na mikakati madhubuti ya usimamizi wa fedha za Umma inayoweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza duniani ikiwa ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabia nchi, mabadiliko ya kiteknolojia na mabadiliko ya kiuchumi.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa Innocent L Bashungwa wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Mwaka wa Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa nchi za Afrika (AAAG) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha mapema leo Desemba 02, 2024.
Mhe. Bashungwa amesisitiza kuwa, uwepo wa mifumo thabiti ya usimamizi wa fedha za Umma, utapunguza gharama za usimamizi, kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wengi zaidi.
Aidha, ametoa wito kwa Jumuiya hiyo kupendekeza mbinu mpya za kuboresha usimamizi wa fedha za umma kupitia matumizi ya teknolojia ya kidijitali ili kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji.
"Niwatake wana Jumuiya kuona namna ya kukuza ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, Sekta Binafsi na Asasi za kiraia, katika usimamizi wa fedha za Umma hasa katika kutekeleza miradi ya maendeleo".Amesema
Naye Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameeleza usimamizi madhubuti wa fedha unasaidia wananchi kujenga tabia ya kulipa kodi kwa hiari ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazofanya vizuri.
Mhe. Nchemba amethibitisha hayo kwa kutolea mifano ya miradi iliyokamilika na inayotekelezwa nchini ikiwemo Bwawa la Kufua Umeme, miradi ya umwagiliaji, miundombinu ya barabara, ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo - Busisi) pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR)
Hata hivyo, Mhasibu Mkuu wa Serikali wa Ufalme wa Lesotho na Mwenyekiti wa Jumuiya ya AAAG, Malehlonolo Mahase ameeleza kuwa, kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo kuna malengo na manufaa muhimu katika usimamizi bora wa fedha za umma na kuimarisha utendaji katika nchi za Afrika.
Awali, Mkutano huo wa umebeba kauli mbiu ya “Kujenga Imani ya Umma katika Mifumo ya Usimamizi wa Fedha za Umma kwa Ukuaji Endelevu”.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.