Na Elinipa Lupembe
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imemuagiza Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya, kuweka mpango mkakati wa kujenga uzio kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za Afya Nchini.
Agizo hilo lilekuja kufuatia ombi la wananchi wakazi wa kata ya Olturumet halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru, kuiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kujenga uzio kwenye hopitali yao ya wilaya ya Olturumet, ili kuongeza usalama wa wagonjwa na mali za hospitali, wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa hospitali ya Olturumet, mradi unaotekelezwa na Serikali kwa gharama ya shilingi milioni 900.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Justine Nyamoga (MB), ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kujenga uzio kwenye hospitali hiyo ya Olturumet lakini kuweka mpango endelevu wa kujenga uzio kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.
"Kutokana na umuhimu wa kuongeza usalama wa wagonjwa, mindombinu, mifumo na mali zote kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya nchini, ni vema Ofisi ya Rais TAMISEMI ikaweka mpango endelevu wa kujenga uzio, ambao utazuia na kuepusha changamoto mbalimbali zinazoweza kuepukika" Amesema Mhe. Nyamoga.
Awali akizungumza kwa niaba wananchi, Diwani wa kata ya Olturumet Mhe. Joseph Tinayo, ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha nyingi zilizotekeleza miradi kwenye kata hiyo, ikiwemo shilingi milioni 900 za mradi huo wa upanuzi wa hospitali unaojumuisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la Maabara, Mionzi na jengo la kuhifadhia maiti na kuiomba serikali kujenga uzio katika hospitali hiyo.
"Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya sita, imefanya kazi kubwa na nzuri, Dkt.Samia ametutendea haki wananchi wa Olturumet, barabara imewekwa lami, majengo yote muhimu yanaongezeka kwa kasi, ombi letu kubwa, hospitali hii ijengwe uzio, ili kuongeza ulinzi na zaidi hadhi ya hospitali yetu" Ameweka wazi Mhe. Tinayo.
Hata hivyo Naibu Kaibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Eng. Rogatus Mativila, amekiri kupokea agizo hilo na kuahidi kulifanyia kazi.
Wajumbe hao wa Kamati, wamefanya ziara ya siku moja ya kukagua utekelezaji wa miradi ya Maendeleo halmashauri ya Arusha, Meru na Longido.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.