Wajumbe wa Kamati ya Siasa mkoa wa Arusha, wametembelea na kukagua hali ya ujenzi wa mradi wa shule mpya ya Msingi ya Emayan kijiji cha Lemanda kata ya Oldonyosambu, mradi uliotekelezwa na Serikali kwa gharama ya shilingi milioni 348.5 kupitia Programu ya SEQUIP
Wajumbe hao licha ya kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo, mradi uliotekelezwa kwa viwango vya ubora unaoendana na thamani ya fedha, ameuagiza uongozi wa kata ya Oldonyosambu, kufuatilia na kuwahimiza wazazi kuwasimamia na kuhakikisha watoto wa kiume wanakwenda shule, watoto ambao mahudhurio yao yanaonekana kuwa ni hafifu ukilinganisha na wasichana, kutokana na jamii za kifugaji kuwapa watoto wa kiume kazi ya kuchunga mifugo muda wa masomo na kushindwa kuhudhuria masomo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Loy Thomas Ole Sabaya, amesema kuwa, uongozi wa kata na vijiji, wanalazimika kuwafuatilia wazazi ambao wanawapelekea watoto wao kuchunga mifugo badala ya kwenda shuleni na kuwachukulia hatua za kisheria kwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bila kujali jinsi zao.
"Ninawataka wazazi wote, wanaowazuia watoto hasa wa kiume kwenda shule na kuwapeleka kuchunga mifugo, kuacha mara moja tabia hiyo na kuwaruhusu watoto hao kusoma kwa kuzingatia malengo ya Serikali ya kusomesha watoto wote, tambueni Serikali imetumia fedha nyingi kujenga shule, viongozi wa kata chukueni hatua kali kwa yoyote anayeleta vikwazo kwa watoto kusoma". Amesema Sabaya
Awali, Shule hiyo ya Emayani, imesajiliwa na tayari wanafunzi wameshaanza kusoma shuleni hapo, shule ikiwa na jumla ya wanafunzi 683, wavulana 295 na wasichana 388.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.