Wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Arusha, wametembelea na kukagua Mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari Kamwanga wilaya ya Longido, na kuagiza mradi huo kukamilika ifikapo tarehe 29 Machi,2024 na kwa viwango vinavyokubalika.
Wakikagua mradi huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Thomas Loy Ole Sabaya, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Longido, kuongeza kasi ya ujenzi ili kukamilisha mradi kwa kuwa mpaka sasa uko nyuma ya wakati kwa miezi sita.
Naye, Mkurugenzi halmashauri ya Longido, Steven Ulaya, amekiri kuchelewa kwa mradi huo, kulikotokana na kuchelewa kupatikana kwa eneo la ujenzi pindi fedha za mridi huo zilipoingia na kuahidi kuendelea kusimamia kwa karibu na mpaka kufikia tarehe 29 Machi mradi huo utakuwa umekamilika.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Enduimet Mwl. Hassan Hassan, amesema kuwa, mradi huo unatekelezwa kwa kiasi cha shilingi milioni 584.2, fedha kutoka Serikali Kuu kupitia mpango wa kuboresha Elimu ya Sekondari Tanzania (SEQUIP).
Amesema kuwa, Mradi huo unajumuisha ujenzi wa jengo la Utawala, vyumba 8 vya madarasa, maabara tatu za somo la Fizikia, Kemia na Baiolojia, Maktaba, jengo la TEHAMA,pamoja na matundu 20 ya vyoo.
Aidha mradi huo ukikamilika unatarajiwa kuboresha mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kupunguza msongamano katika shule zingine za Sekondari.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.