Na. Zainabu Ally - Arusha
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) jana tarehe 16.11.2023 limemuaga rasmi aliyekuwa Kamishina wa Uhifadhi Dkt. Allan Kijazi baada ya kumaliza utumishi wake katika shirika hilo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA Jenerali Mstaafu George Waitara amempongeza Kamishina Mstaafu Dkt. Kijazi kwa kuliletea shirika hilo mageuzi na mafanikio makubwa katika kipindi cha uongozi wake akitaja kuwa ni sehemu ya matokea ya uongozi ulio imara na thabiti.
"Ulishiriki kikamilifu katika kuleta mabadiliko makubwa ya kimfumo ndani ya shirika hususani katika kubadili muundo wa utendaji kutoka wa kiraia na kuwa wa kijeshi, mfumo ambao umeleta ufanisi, nidhamu, uwajibikaji na uzalendo katika utendaji ,hivyo haitakuwa rahisi kuelezea historia ya TANAPA bila kukutaja kwa mchango wako huo mkubwa"
"Kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini TANAPA ninakupongeza sana kwa kustaafu kwa heshima kwani kazi yako ilikuwa ngumu sana hasa katika wakati wa ujangili uliotishia kutoweka kwa wanyama adimu kama vile Faru pamoja na kupambana na uhalifu mwingine ndani ya hifadhi zetu. Pia nakupongeza kwa uvumilivu wako na msimamo uliokuwa hata kama maamuzi ya Bodi ya Wadhamini yalitofautiana na TANAPA ulisimama na kuonesha dira iliyopelekea kupata mwelekeo sahihi.
Akitoa salamu zake za kwa heri Kamishna Mstaafu wa Uhifadhi Dkt. Kijazi aliwashukuru Marais wa awamu zote 3 aliofanya nao kazi na kumpandisha kushika nyadhifa kubwa na muhimu katika Taifa.
"Alisema, kwa upekee sana nawashukuru marais wa awamu zote walioniteua ili kulitumikia Taifa letu, hakika kwangu ni heshima kubwa mnoo lakini hayo yote yametokana na ushirikiano, mshikamano na kazi nzuri ambayo mliifanya na kuiwezesha TANAPA kung'aa na mimi kama kiongozi wake niweze kutambuliwa na viongozi wa ngazi na kitaifa."
"Nina waomba endeleeni kuwa na mshikamano huo katika kufanya kazi zenu za kila siku huku, hekima na busara vikitawala pamoja na kuwepo kwa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya uhifadhi na utalii maana umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu."
Awali, akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John V.K. Mongella alimpongeza Dkt. Kijazi kwa kupata mafanikio makubwa katika utumishi wa umma, na mkoa wa Arusha unajivunia mchango mkubwa wa TANAPA katika kukuza pato la mkoa na kwa mtu mmoja mmoja.
"Nichukue fursa hii adhimu kukupongeza kwa mafanikio yako makubwa katika utumishi wa umma na sisi kama mkoa wa Arusha tunatambua mchango wako kupitia TANAPA ambao ni mdau mkubwa wa maendeleo nchini na hasa katika mkoa wetu kwa kuwa makao makuu yake yapo hapa."
Kaimu Kamishina wa Uhifadhi TANAPA Juma Kuja, alisema kuwa Shirika linathamini na litaenzi mazuri yote aliyoyafanya katika uongozi wake katika kuimarisha uhifadhi na kukuza utalii.
Hafla na tafrija makhususi ya kumtakia maisha mema baada ya utumishi uliotukuka wa Kamishna wa Uhifadhi Mstaafu Dkt. Allan Kijazi ilifanyika jana jioni tarehe 16.11.2023 katika Ukumbi wa AIM Mall mtaa wa Majengo jijini Arusha.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.